WATAKATIFU
UFAHAMU
JUU YA WATAKATIFU
1. Jinsi ya upatikanaji wa mmoja kuitwa Mtakatifu.
Maana ya neno Mtakatifu
Katika Agano la Kale Mungu pekeyake
aliitwa Mtakatifu (rej. Isaya 6:3). Pili neno Mtakatifu katika Agano la Kale
lilitumika pia kwa wale waliowekwa wakfu kwa ajili ya utumishi wa Mungu (rej.
Law 17:1).
Tukija katika
Agano Jipya, Mtakatifu ni neno lenye asili ya lugha ya Kigiriki “hagios” linalotumika katika Maandiko
Matakatifu hasa Agano Jipya kuwaonesha
wafuasi wa Yesu. Wote wale waliosadiki na kubatizwa walijiunga na “ukoo mteule,
makuhani wa Mfalme, taifa takatifu na watu wake Mungu mwenyewe”(1Petro 2:9).
Mtakatifu ni neno pia linalowaelezea waamini walioishi kabla ya wakati wa Yesu (Mathayo 27:52). Pia neno hili
linatumika kwa wale walioingia katika Agano
Jipya na Yesu Kristo (Wafilipi 1:1). Mtakatifu kwa upande mwingine ni kama jina mbadala la
waamini Wakristo wa Kanisa la
mwanzo. Kwa mfano, Mtume Paulo alipenda kuwaita “watakatifu” wale wote aliokuwa
akiwaandikia. Warumi 1:7, Waefeso 1:1, 1Kor
1:2, 2Wakorintho 1:1.
Kupanuka kwa
dhana ya Mtakatifu
Mtakatifu ni mtu
yule aliyeko mbinguni ambaye anawaombea watu na Kanisa lililoko duniani wapate
mahitaji yao. Mtu huyo anakuwa ametuzwa heshima na umati mkubwa wa watu na
ametambuliwa na kanisa. Aidha,watakatifu ni kusanyiko kubwa sana la wazaliwa wa
kwanza wa Mungu ambao majina yao yameandikwa mbinguni. Hizo ni roho za watu
waadilifu waliofanywa kuwa watakatifu ambao wamejenga kusanyiko kubwa sana la
watu hai ambao wamejitakatifuza kwa damu ya Yesu Kristo na kwa neema yake,
katika kufuata nyayo zake na wakawa wametekeleza kazi inayompendeza Baba. Miongoni
mwao wakiwa mashahidi ambao wamekuwa daima chemchemi na asili ya kujifanya upya katika nyakati
zilizokuwa ngumu zaidi, ya historia ya
kanisa.
Mashahidi ndio wale
waliokubali kifodini kuliko kuachilia imani yao kwa Mungu. Hawa ni mashahidi wa
Mungu. Kwa hiyo wote hao wakiwa wameungana kabisa pamoja na Kristo wanashiriki
kulijenga kanisa kwa uthabiti zaidi katika utakatifu. Hapa ndipo tunapomkumbuka
kwa namna ya pekee kabisa Stefano ambaye ndiye anayetajwa kama shahidi wa
kwanza (Mdo 7: 52-60).
Nani anayerudisha jina toka
mbinguni kuwa mtu fulani ni Mtakatifu?
Ni kwa njia ya ufunuo ambao
Kanisa huupata kutoka kwa Mungu. Mungu anapotupa ufunuo wake kimsingi anakuwa
anajibu yale maombi ambayo sisi binadamu tulioishi na mtu husika tunakuwa
tuliyatuma kwake. Kwa kifupi basi hiyo shughuli nzima inafanywa na Mungu
mwenyewe kupitia Kanisa lake na kwa namna ya pekee viongozi wa Kanisa akiwemo
baba Mtakatifu.
Historia ya kumtangaza mtu kuwa
mtakatifu
Jambo hili linayo historia yake.
Katika historia ya kanisa hapo mwanzo wafiadini walipewa mara moja heshima ya
pekee kwa sababu walikuwa wameishuhudia imani yao kwa Bwana wetu Yesu Kristo.
Mtume Peto na Paulo wanatoa ushuhuda huo baada ya kufa kifo dini kati ya mwaka
64 hadi 67 baada ya Kristo. Ndipo basi kuanzia karne takribani ya nne hivi wale
ambao hawakuwa wafiadini, nao walianza kupewa heshima kama hiyo hiyo. Hawa
walikuwa ni mashujaa waliovumilia maisha magumu na yenye taabu, kama vile wakaa
pweke, wamonaki, maaskofu na wale waliojihusisha na kutatua mafundisho rasmi ya
dini yetu.
Ndipo basi baadaye, majina ya
watakatifu hao wake kwa waume, yaliorodheshwa na hivi kila askofu alikuwa na
orodha ya watakatifu waliokufa katika jimbo lake. Mambo yaliendelea hivyo mpaka
katika karne ya kumi, ambapo Papa Yohane wa Kumi na tano alianza kuyachunguza
yeye mwenyewe maisha ya mkristo aliyekuwa ameishi kishujaa katika fadhila kabla
ya kuliandika jina lake katika orodha ya watakatifu. Tangu hapo uchunguzi
ukazidi kufanyika kwa uangalifu zaidi. Hatimaye kuanzia karne ya kumi na tatu,
akawa ni Papa peke yake ndiye aliyekuwa
na uwezo wa kumtangaza mtu kuwa mtakatifu.
2. Hatua zinazofuatwa katika kumtangaza mtu kuwa
Mtakatifu
Tangazo la mtu fulani kuwa mtakatifu
ni lazima lipitie hatua tatu muhimu ambapo bila hizo mtu hawezi kutangazwa kuwa
mtakatifu. Ikumbukwe kuwa hatua hizo hupitiwa baada ya kuwa mtu amekufa na si wakati akiwa hai.
Hatua ya kwanza ni ile ya mtumishi wa Mungu.
Hii ni hatua ya
kupeleka jina la mtu huyo mnayetaka atangazwe kuwa mtakatifu kwenye Idara
maalumu inayoshughulikia utangazaji wa wenye heri na watakatifu, Idara hiyo
inayo makao yake makuu huko Roma. Lengo la kupeleka jina hilo ni kutaka
kuchunguza maisha ya mtu huyo kwa ukaribu zaidi. Uchunguzi huo hufanywa kwa
kuhusisha maoni ya wananchi wote kwani mtu huyo atadaiwa kuwa aliishi vema sio
tu na Wakatoliki au Wakristo bali na wananchi wote au jamii nzima ya watu
waliokuwa wakimzunguka.
Hii ni shughuli inayochukua miaka mingi kidogo kwani huhitajika mashahidi
waliomjua Mkristo huyo ili waweze kuhakikisha kabisa tena kwa mifano ushujaa
wake. Shughuli hii husimamiwa na askofu wa jimbo alimokuwa akiishi Mkristo
huyo. Ripoti hiyo iliyotumwa huko Roma huchunguzwa kwa makini na hata kutaka
kujua kama kuna miujiza yeyote ambayo imefanyika kupitia maombezi yake mtu
huyo. Ndipo basi kama wakuu hao wa Idara wakiona kuwa hayo yote yamethibitishwa
bila ya shaka yeyote, hapo ruhusa rasmi hutolewa ya kumwita Mkristo huyo
“Mtumishi wa Mungu”. Na hivyo ndivyo inavyokamilika hatua hiyo ya kwanza.
Hatua ya pili ni ile ya Mwenyeheri:
Ni baada ya miaka
kadhaa hatua hii ya pili huweza kuidhinishwa. Hii ni baada ya kurudia upya
mambo yote yaliyokwishafanywa katika hatua ya kwanza yaani, mashahidi
wanahojiwa ambao wanaweza kuthibitisha kinaganaga, na kama kwa maombezi ya
Mtumishi wa Mungu, sala zilisikilizwa na miujiza ilitendeka; aidha, watu
wengine huhojiwa tena ili waweze kuthibitisha jinsi Mtumishi wa Mungu
alivyoishi kifadhila kwa ushujaa mkubwa. Kama haitoshi ushahidi huo na maelezo
hayo yote lazima yaandikwe hata kiasi kinachofikia maelfu na maelfu ya kurasa.
Hapo sasa ndipo kamati kuu huundwa na wahusika wa kamati huchaguliwa na Papa
mwenyewe ili kuweza kufanya majadiliano ya kina sana juu ya fadhila na miujiza
ya Mtumishi huyo wa Mungu.
Mwisho wa yote ni juu ya Papa mwenyewe
baada ya kuyasoma hayo yote na kusali sana tena sana ili kuyajua mapenzi ya
Mungu, kuamua kama anaweza kuikubali hatua ya pili au hapana. Kama ndivyo basi
huyo, Mtumishi wa Mungu, hutangazwa kuwa “Mwenye Heri”.
Hatua ya tatu na ya mwisho ni
kutangazwa mtakatifu. Kisha kutangazwa kuwa Mwenye Heri
Kanisa na wanakanisa wote huombwa kusali kwa kumwomba huyo mwenye heri miujiza
itendeke kwa jina lake. Hapa Kanisa hutumia haki ya binadamu ya kumuuliza Mungu
kitu na kusuburi jibu.
Hii ni haki ambayo binadamu anakuwa
nayo ilimradi tu hana nia ya kumjaribu Mungu. Muujiza wowote unaofanyika kwa
jina la Mwenye Heri huyo huripotiwa
kwenye Idara husika, lakini kila tukio linalodaiwa kuwa ni muujiza huchunguzwa
tena na tena kwa ukamilifu kama kweli ni muujiza.
Ni dhahiri kwamba kazi hii huchukua
miaka mingi sana kwani mikutano mingi hufanyika tena na tena, na majadiliano
huwa ni mengi na watu wengi sana huhojiwa kuhusiana na suala hili. Ni ukweli kuwa Kanisa huwa ni gumu katika
kuipokea miujiza, kusudi lisifanye
makosa ya kutangaza tukio fulani kuwa ni muujiza wakati sio. Kwa kifupi Kanisa
halitaki kujutia au kutangua kitu kilichotangazwa tayari.
Ndipo basi, miujiza saba ikitokea kwa
jina la Mwenyeheri husika na kukubalika na Kanisa, Kanisa hujua kwamba Mungu
amewabainishia kwamba mtu husika amefika katika makao matukufu ya Mungu
mwenyewe. Hata hivyo mwenye kutoa uamuzi wa mwisho ni Papa mwenyewe ambaye, kwa
mara nyingine anasali sana tena na tena ili apate kuyajua mapenzi ya Mungu
katika jambo hilo. Kama baada ya shughuli hizo zote anaamua kuendelea, bila
kipingamizi, basi hapo ndipo Papa katika Ibada maalumu humtangaza Mwenyeheri
huyo kuwa Mtakatifu. Hivyo ndivyo zinavyokamilika hatua tatu za mtu kutangazwa
kuwa Mtakatifu.
3.
Kuna utofauti gani kati ya utakatifu na
wokovu?
4.
Ni vigezo vipi vinavyomfanya mtu aitwe
mtakatifu?
5.
Juu
ya Baba Mtakatifu
I.
Je,
baba Mtakatifu ni Mtakatifu?
II.
Kuna
utofauti gani kati ya utakatifu wa baba Mtakatifu na utakatifu wa watakatifu
ambao kanisa huwakumbuka kila siku na kuadhimisha misa kwa heshima yao?
III.
Kuna
umuhimu gani wa kukiita kiti cha baba Mtakatifu kitakatifu wakati yeye si
mtakatifu?
IV.
Je,
kuna watakatifu walio hai?
V.
Kwa
nini Kanisa kuwakumbuka watakatifu wachache tena kujirudia mwaka hadi mwaka,
hakuna walioishi kitakatifu zaidi ya hao?
VI.
Tarehe
au siku ambayo Kanisa hukumbuka watakatifu inamaanisha nini? Kifo cha mtakatifu
au kupewa utakatifu?
VII.
Kazi
ya watakatifu ni nini?
6.
Kwa
nini mababu zetu wa kwanza ambao waliishi vizuri hapa duniani kama akina
Ibrahimu na Musa hawajatangazwa watakatifu?
7.
Juu ya Masalia ya watakatifu
I.
Je, ni halali masalia ya watakatifu
kuwekwa altareni?
II.
Je, masalia
ya watakatifu altareni si ushirikina?
III.
Kwa nini
Wakatoliki wanayaabudu masalia yanayowekwa altareni?
Tofauti kati ya utakatifu na wokovu?
Tofauti iliyopo kati ya utakatifu
na wokovu ni ndogo sana, nayo ni hii kuwa mtu hawezi kutangazwa mtakatifu kama
kwanza hajaokoka.
Hii ni kusema kuwa, baada ya kuwa
mtu ameokoka yaani baada ya kifo chake na kupewa tunu na Mwenyezi Mungu ndipo
hapo kanisa kwa kuangaziwa na Mungu huanza mchakato wa kumtangaza mtu husika
kuwa Mtakatifu. Kwa maelezo hayo basi bado tunabaki palepale kuwa watakaookoka
watakuwa ni wengi na pengine sio wote watakaotangazwa kuwa Watakatifu.
Kila aliye Mtakatifu ni lazima
awe kwanza ameokoka lakini haya yote yanatokea baada ya kifo chake na sio
kabla. Ni ukweli pia kuwa miongoni mwa watakaookoka ndio watakaotambuliwa kuwa
ni Watakatifu. Kila atakayeokoka ni Mtakatifu ingawa anaweza kuwa ametangazwa
kuwa Mtakatifu au hajatangazwa kuwa Mtakatifu.
Hata hivyo kwa ujumla maneno haya
mawili yaani wokovu na utakatifu, hayapingani kwa yenyewe kwani yote
yanamaanisha tunu, thawabu au heko ambayo mmoja anatunukiwa na Mungu baada ya
kuwa aliishi vizuri pindi alipokuwa hapa duniani.
Ni vigezo vipi vinavyomfanya mtu aitwe Mtakatifu
Vigezo vya mmoja kutangazwa kuwa
Mtakatifu ni kuishi vema hapa duniani, kufa vema na hatimaye kutunukiwa thawabu
hiyo kubwa kabisa na Mungu mwenyewe. Kila mmoja anayo nafasi ya kuwa Mtakatifu
hapo baadaye kwani nafasi hiyo haijatengwa kwa ajili ya mapapa tu, maaskofu,
mapadre, masista n.k, la hasha nafasi hiyo ni ya kila mmoja ilimradi anaishi
vema hapa duniani. Ndio maana ukisoma katika litania ya watakatifu wote utapata
watakatifu mapapa, maaskofu, manabii, mapadre, watawa, walei na wengine chungu
mzima.
Hapa Mwenyeheri Yohane wa XXIII
atakayetangazwa kuwa Mtakatifu hapo kesho alikuwa na msemo mmoja kuwa
“Inawezekana kuwa Mtakatifu wakati wa kushika fimbo ya askofu, lakini vile vile
inawezekana kuwa Mtakatifu wakati wa kushika mkononi ufagio”.
Ndipo sasa ukienda mbali zaidi katika
suala hili hili utagundua kuwa sio Wakristo tu ndio wanaoweza kuwa Watakatifu
bali ni hata Waislamu, Wabudha, Wapagani na wote ambao hawatakuwa wamelipata
neno la Mungu yaani kufikiwa na Kristo. Hii ni kwa sababu kila mtu atahukumiwa
kadiri ya dhamiri yake, yaani kadiri mtu huyo alivyoisikiliza dhamiri hiyo.
Mtume Paulo anatuhabarisha hayo anaposema kuwa “kuisikiliza dhamiri ni
kumsikiliza Kristo mwenyewe” haya yanapatikana katika Rum 2:15-18 na 2Tim
4:1-4.
1. Maelezo juu ya Baba Mtakatifu na utakatifu wake. Mfano
halisia wa hayati baba Mtakatifu Yohana Paulo II ambaye Kanisa limemtangaza
rasmi kuwa mtakatifu baada ya kifo chake, hata hivyo kutangazwa huko kumepitia
hatua zote za kutangazwa mtakatifu.
Tufahamu kuwa,Tunatumia neno mtakatifu
tumtajapo Papa au kiongozi wetu mkuu kwa mfano Baba Mtakatifu Benedikto wa XVI,
Baba Mtakatifu Fransis n.k kwa sababu ya kazi anayoisimamia au aliyokuwa
akiisimamia, na si utakatifu wake yeye binafsi.
Hapa naomba nieleze japo kwa
kifupi, kuhusu Baba Mtakatifu au Papa ni nani, sawia na mamlaka yake katika
Kanisa Katoliki. Papa ni wakili wa Yesu
Kristo, Halifa wa Mtume Petro, Mkuu wa Kanisa Katoliki, Askofu wa jimbo la
Roma. Zaidi ya hapo Baba
Mtakatifu ni Rais wa Nchi ndogo ya Vatikani.
Mintarafu madaraka ya Baba
Mtakatifu, kwa jina lile la “Mwandamizi wa Petro” madaraka ya Baba Mtakatifu
yachukuliwa kuwa yatoka kwa Mtume Petro aliyewekwa na Yesu mwenyewe kuwa
“mwamba juu yake Kanisa lilijengwa” Nami nakuambia: Wewe ndiwe Petro na juu ya
mwamba huu nitalijenga kanisa langu, wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme
wa mbinguni; na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa
mbinguni, na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni (rej.
Mt 16:18-19; Lk 22:31-32).
Aidha ni Petro aliyepewa jukumu la kuwachunga na kuwalisha
Kondoo wa Yesu “… Yesu akamwambia Simoni Petro, Je, Simoni wa Yohane,
wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia, Naam, Bwana wewe wajua kuwa nakupenda.
Akamwambia, Lisha kondoo wangu. Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohane,
wanipenda?
Akamwambia, ndiyo, Bwana, wewe
wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu. Akamwambia mara ya tatu,
‘Simoni wa Yohane, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya
tatu, ‘wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya
kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo wangu” (rej. Yn 21:15-17).
Maana ya fundisho la Yesu ni wazi.
Hapa kondoo ni wale wote watakao mwamini au wafuasi wa Yesu Kristo, na hivi
maana yake ni kwamba, Mtume Petro aliwekwa kuongoza na kutawala waamini na
wachungaji wao. Huo ndiyo wajibu wa kichungaji aliokabidhiwa Mtume Petro na
Yesu Kristo, ndiyo maana akakabidhiwa na ufunguo wa mamlaka ya kufunga na
kufungua ya duniani naya mbinguni (rej. Mt 16:19). Wajibu huo wa kichungaji wa
Mtume Petro ndiyo kwa sasa unaendelezwa na Baba Mtakatifu. Hivyo basi, Papa ni
jaji mkuu wa mambo yote ya imani na maadili katika kutamka na kutumia mamlaka
yake yasiyopingika.
Lakini wapo watu wanaopotosha kwa
kusema kwamba ‘mwamba’ ule ni jiwe
dogo. Lakini sisi twasema kwamba si hivyo kwa kuwa “Petros” kwa lugha ya Kigiriki, “Petra” kwa lugha ya Kilatini na “Kefas” kwa lugha ya Kiebrania, kila mara maana yake ni mwamba
mkubwa.
Pia, wapo wanaosema kwamba ahadi
hiyo ya Yesu ilikuwa kwa Simoni Petro tu, wala haiwahusu wale waliomfuata
Petro. Lakini maelezo Katoliki yasema kwamba hiyo haiwezekani kabisa: mwamba wa
Kanisa lazima uwe mwamba wa kudumu. Yaani katika maana ya kurithishwa kwa
waandamizi wengine watakaofuata baada ya kifo cha Petro. Tukisema kwamba kauli ya Yesu ilimlenga Petro peke yake basi
ingebidi huyo Petro asife au Kanisa nalo life baada ya kifo chake.
Sisi tunaamini kwamba Kanisa
Katoliki ni la kweli kwa sababu limejengwa juu ya Mwamba wa Upapa na linakubali Uchungaji
wa upapa. Kanisa Katoliki lipo tangu Papa wa kwanza, yaani Petro. Katika karne
ya kwanza wapo mahalifa wake, yaani Linus, Anakleti, Klement na Evaristi.
Zaidi, tunayo orodha ya mapapa wote mpaka Fransis aliye Papa kwa sasa.
Tangu halifa wa kwanza wa Bwana
wetu Yesu Kristo, yaani Mtume Petro, hadi leo hii tunao Mapapa 266, ikiwa ni
pamoja na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa XVI ambaye ni wa 265, na Papa
anayeliongoza Kanisa Katoliki kwa sasa ambaye ni Baba Mtakatifu Fransis yeye ni
wa 266.
Yesu alimchagua Simoni Petro kuwa kiongozi
mkuu na wa kwanza wa Kanisa lake. Petro
aliliongoza Kanisa tangu mwaka 33 baada ya kupaa kwa Yesu mbinguni mpaka mwaka
67 alipokufa kifo dini. Mtume Petro, kufuatana na ushahidi dhahiri alikufa Roma,
na kaburi lake liligunduliwa chini ya Altare Kuu ya Kanisa la Mtakatifu Petro
huko Roma.
Tangu hapo utumishi huo (kiti
hicho) umekuwa ukirithiwa bila kukatishwa mpaka leo hii, ambapo tunaye Papa wa
266 tangu wakati wa Petro. Tukisema kwamba kauli ya Yesu ilimlenga Petro peke
yake basi ingebidi huyo Petro asife au Kanisa nalo life baada ya kifo chake.
Lengo la Yesu lilikuwa ni kutunza umoja wa Kanisa lake, hivyo Papa ni ishara ya
umoja huo. Tukumbuke kwamba bila ya
Papa hakuna ukweli wala umoja. Matokeo ya kumkana ni madhehebu maelfu na maelfu
ya Kikristo yaliyojitokeza katika historia ya Kanisa.
Huo ndio ufupisho kuhusu Baba
Mtakatifu na wadhifa wake katika Kanisa Katoliki.
Je,
papa au baba Mtakatifu ni Mtakatifu na kwa nini tunakiita kiti cha papa kitakatifu?
Kumbe basi tunaposema Papa au baba Mtakatifu hatumaanishi
kuwa yeye ni Mtakatifu la hasha bali kilichokitakatifu ni kiti anachokikalia
huyo baba Mtakatifu. Kiti hicho ni Kitakatifu kwa sababu Yesu Kristo mwenyewe
aliye si tu mtakatifu bali ni utakatifu wenyewe alimteua Petro Mtume wake kama
Papa au baba Mtakatifu wa kwanza kukalia kiti hicho cha kuliongoza Kanisa.
Ndio kusema kuwa Papa anaitwa Baba Mtakatifu si kwa nafsi
yake kama mwanadamu bali ni cheo na dhamana ya kazi yake kama mwakilishi wa Mungu
katika Kanisa. Hivyo utakatifu wa Papa siyo hasa wa maisha yake binafsi bali ni
wa kazi yake.
Kama kazi ya Kanisa zima ni kutakatifuza waamini basi huyo
mwenye dhamana ya kusimamia kazi zote za kutakatifuza ni Mtakatifu. Anaweza
akawa mtakatifu au asiwe mtakatifu hilo litategemea na neema za Mungu na bidii
yake mwenyewe (rej. 1Kor 9: 26-27), lakini si kwamba ana tiketi ya kwenda
mbinguni moja kwa moja. Ila vile vile anayo nafasi nzuri zaidi ya kuwa
mtakatifu kwa vile ukaribu na Mungu anaokuwa nao.
Ni kwa sababu hiyo basi kati ya mapapa 264 waliokwishapita si
wote waliotangazwa kuwa ni watakatifu bali ni wachache tu. Na hii ni
kudhihirisha kuwa wapo mapapa wengine ambao wameshindwa kupewa tunu hii ya
utakatifu na mwenyezi Mungu au wamepewa tunu hiyo lakini Kanisa bado
haliwatambui kama ni watakatifu. Hivyo basi hakuna ukweli wowote kuwa kila
atakayekuwa baba Mtakatifu ni lazima awe Mtakatifu. Vigezo na masharti ni
muhimu kuzingatiwa katika hili na tena huwezi kuwa Mtakatifu kama hujapitia
hatua zile tatu za kuwa Mtakatifu, yaani kutangazwa kama mtumishi wa Mungu,
mwenyeheri na hatimaye kutangazwa rasmi kama Mtakatifu.
Hata hivyo kwa upande wa papa Yohane Paulo wa II, usijali
kwani hatimaye Baba Mtakatifu huyu ametimiza vigezo na hivyo na hivyo Yohane
Paulo wa Pili kuitwa Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili.
Kuna
utofauti gani kati ya utakatifu wa baba Mtakatifu na utakatifu wa watakatifu
ambao Kanisa huwakumbuka kila siku na kuadhimisha misa kwa heshima yao?
Kama tulivyoona kwamba, utakatifu wa baba mtakatifu si wa
kwake yeye mwenyewe binafsi bali ni wa mambo anayoyasimamia. Kwa upande
mwingine utakatifu wa watakatifu ambao mama Kanisa huadhimisha misa kwa heshima
yao kwa mfano akina Mtakatifu Augustino akina Mtakatifu Katalina wa Siena,
Mtakatifu Yohane Bosco, Dominiki Savio na wa wengine wengi ni utakatifu wao
binafsi. Yaani niwatakatifu katika maana halisi ya utakatifu. Na hawa wapo
mbinguni.
Tukija kwa upande wa Baba Mtakatifu, kwa mfano sasa tunaye
papa Fransis, tunamwita Baba Mtakatifu Fransis kutokana na dhamana
anayoishikilia yaani ya kuliongoza Kanisa na wala si utakatifu wake yeye
binafsi kwa kusema hivyo hatukatai kwamba yeye si au hawezi kuwa mtakatifu la
hasha!
Tunachomaanisha kwamba naye lazima kwanza afe kisha kufa kama
kuna ulazima wa kumtangaza mtakatifu ndipo naye afuate mchakato ule ule wa mmoja
kutangazwa Mtakatifu.
Laiti tungewaita mapapa Mababa Watakatfu tukimaanisha
utakatifu hao binafsi basi kusingekuwa na haja ya wao kufuata hatua hizo ambazo
nimekwisha zitaja ili kuwatangaza. Kwa kifupi ni kwamba hatua za kumtangaza
mmoja kuwa mtakatifu ni zilezile kwa watu wote haijalishi mhusika alikuwa papa
au mwanajeshi au rais nk.
Ndipo basi katika mchakato kama huu wa mmoja kutangazwa kuwa
Mtakatifu hakuna undugu au rushwa. Hakuna kusema labla kwa sababu mmoja alikuwa
Papa basi apate upendeleo, haya ni kinyume na maadili ya Kanisa letu lenye sifa
ya Utakatifu ndani yake. Mchakato huu mzima unahusisha sala kwa Mwenyezi Mungu
na ndanimo hatutegemei kuona upendeleo, urafiki, undugu, urangi, ubara, ujinsia
au ubaguzi wa aina yeyote ile. Ni Kanisa ndilo linalojulishwa na Mungu kwa
ufunuo kwamba mtu fulani aliyeishi vizuri hapa duniani ameutafuta uzima wa
milele kwa mafanikio, na hivi mtu huyo hanabudi kuwekwa kama mfano mbele ya
wengine wanaoendelea kutafuta kwa mafanikio uzima wa milele.
Kuna
umuhimu gani wa kukiita kiti cha baba Mtakatifu kitakatifu wakati yeye si
mtakatifu?
Umuhimu wa kukiita kiti cha baba Mtakatifu kitakatifu, hata
kama tunasema kuwa si kila anayekalia kiti hicho kitakatifu ni lazima awe
Mtakatifu. Ninasema upo umuhimu kwa sababu yeye aliyempa Petro kiti hicho kwa
mara ya kwanza, si tu ni Mtakatifu bali yeye ni utakatifu wenyewe.
Je,
kuna watakatifu walio hai?
Hakuna Mtakatifu aliyehai ndugu yangu. Kama nilivyokuambia
kuwa ili mmoja atangazwe kuwa Mtakatifu ni lazima apitie hatua tatu yaani
kutangazwa kama mtumishi wa Mungu, Mwenyeheri na hatimaye kutangazwa rasmi kama
mtakatifu, halafu basi hakuna hatua yeyote kati ya hizi ambayo mmoja anaweza
kuipitia akiwa angali hai. Ni lazima kufa kwanza ndipo michakato
mingine yote huweza kufuata. Ila kuna watu wengi wanaouishi utakatifu (maisha
matakatifu) hapa duniani.
Mmoja anayetangazwa Mtakatifu
hutangazwa sio kabla, bali ni baada ya kufa na maisha yake kuchunguzwa sana
kama Maandiko Matakatifu yenyewe yanavyotushauri (rej. Ebr 13:7-9a). Hapa, waamini tunapewa
ruhusa kuwakumbuka wale waliotutangulia katika imani kwa kuchunguza sana mwisho
wa mwenendo wao kusudi tuige imani yao kwa vile tunayepaswa kumtumikia ni Yesu
Kristo ambaye ni yeye yule, jana, leo na hata milele. Kwa maana hii basi, jinsi
walivyotumikia wenzetu inaweza kutufaa sisi pia ambao bado tunaishi hapa
duniani. Hao hutangazwa watakatifu kama Biblia inavyosema baada ya kufa kwao
kwani ndipo tabia yao halisi ya binadamu huwa imepita picha kamili (rej. YbS 11:27b-28).
Ndugu zangu, hata hivyo utakatifu si wito wa watu wachache,
sisi sote tunaalikwa kuwa watakatifu. Na utakatifu wenyewe tunaanza kuutafuta
hapa hapa duniani. Maana yake tungalibado hai. Isipokuwa, Kanisa pamoja na
kutuhimiza kuuchuchumalia utakatifu uliowito wetu sisi sote halijawahi kamwe
kumtangaza mtu ambaye bado yuko hai kuwa Mtakatifu. Kwa nini? Kwa sababu, hujafa hujaumbika!
Ifahamike pia kuwa
hata kuokoka hakuwezekani tunapokuwa
duniani hapa. Ukweli ni kwamba kuokoka kadiri ya Maandiko Matakatifu kunatokea
baada ya kuwa safari ya hapa duniani imekwisha yaani baada ya kifo na sio
vinginevyo. Tunaweza kuona kwamba Biblia inataka kuonesha kuwa kuokoka halisi
ni kilele cha wokovu wetu, ni kuurithi uzima wa milele, ni kumwona Mungu kama
alivyo kama inavyosomeka katika Mdo
15:11; Rum 5:9-10; na Ebr 12:25.
Ikumbukwe kuwa kwa mtu kuniingilia mimi niliye Mkristo na
tena Mkatoliki na kuniambia kuwa yanipasa kuokoka ni sawa na kukiona kibanzi
kwenye jicho langu na kusahau gogo lililo kwenye jicho lake. Ni nani basi
aliyeokoka hapa duniani? Bila shaka hakuna ila sote tunauelekea huo wokovu
ambao unakamilika kwa hatua tatu yaani;
Mosi; ni hatua ya kubatizwa au kuzaliwa upya. Hatua ya pili ni ile ya
kuyaishi maagano ya ubatizo yaani kuutafuta uzima wa milele kwa maisha ya kila
siku. Hatua ya tatu ni ile ya kupokelewa mbinguni kama mshindi wa
vita na kuvikwa taji ya ushindi yaani kupewa na Mungu uzima wenyewe.
Ninasema hivyo kwa makusudi mazima kwamba njiani mambo
yanaweza kugeuka na kuwa vile ambavyo sisi hatukutegemea. Hapa ikumbukwe kuwa
mambo yanaweza kuanza vema lakini mwisho wake ukawa ni mbaya au kinyume chake
pia. Tukumbuke mfano mdogo tu ambao tunauweka kwa vipimo vya kibinadamu huu ni ule wa Yuda, mtume wa Yesu Kristo na
mweka hazina wa mitume na wafuasi wa Yesu aliyeanguka kwenye kishawishi cha
mali akaishia kujinyonga na kupasuka tumbo (rej. Mdo 1:17-20). Je, kama mtume
huyu angejigamba alipoishi hapa duniani na kujiita aliyeokoka ingekuwaje
kuanguka dhambini, tena kwa nafasi nyeti kama ile aliyekuwanayo.Waswahili
husema kwamba usitukane mamba kabla hujavuka mto. Maandiko Matakatifu pia
yanatuambia wa kwanza anaweza kuwa wa mwisho na wa mwisho anaweza kuwa wa kwanza
(rej. Mt 19:30, Mk 10:31, Lk 11:26) na ndipo tunapoaswa kwamba kwa aliyeanza
safari ya kuutafuta uzima wa milele basi avumilie na yule atakayevumilia mpaka
mwisho ndiye atakayeokoka.
Kwa hivi hakuna anayeweza kuitwa Mtakatifu akiwa angali bado
hai hapa duniani na wala hakuna anayeweza kuitwa aliyeokoka akiwa hapa duniani.
Sisi sote tupo safarini kuuelekea huo utakatifu, kuuelekea huo wokovu, hivyo ni
baada ya kifo ndipo mmoja anaweza kuwa Mtakatifu au aliyeokoka.
Kwa
nini Kanisa huwakumbuka watakatifu wachache tena kujirudia mwaka hadi mwaka,
hakuna walioishi kitakatifu zaidi ya hao
Itambulike kuwa dadi ya watakatifu tokea kuumbwa kwa
ulimwengu ni wengi sana ila wale wanaotambuliwa na Kanisa ndio wachache. Hili
linatokana na historia ya kutangazana watakatifu kama nilivyokueleza hapo
awali. Nimeeleza kuwa katika historia ya kanisa hapo mwanzoni wafiadini
walipewa mara moja heshima ya pekee kwa sababu walikuwa wameishuhudia imani yao
kwa Bwana wetu Yesu Kristo wakati walipomfia. Walikuwa na hakika kabisa kwamba wafiadini hao
walikuwa pamoja na Yesu mbinguni. Ni kuanzia karne takribani ya nne hivi wale
ambao hawakuwa wafiadini, nao walianza kupewa heshima kama hiyo hiyo.
Kumbe basi baadaye, majina ya
watakatifu hao wake kwa waume, yaliorodheshwa na hivi kila askofu alikuwa na
orodha ya watakatifu waliokufa katika jimbo lake. Mambo yaliendelea hivyo mpaka
katika karne ya kumi, ambapo Papa Yohane wa Kumi na tano alianza kuyachunguza
yeye mwenyewe maisha ya Mkristo aliyekuwa ameishi kishujaa katika fadhila kabla
ya kuliandika jina lake katika orodha ya watakatifu. Tangu hapo uchunguzi
ukazidi kufanyika kwa uangalifu zaidi. Hatimaye kuanzia karne ya kumi na tatu,
akawa ni Papa peke yake ndiye aliyekuwa
na uwezo wa kumtangaza mtu kuwa mtakatifu.
Ni kutokana na historia hiyo, si kila
aliyetunukiwa cheo cha utakatifu na Mungu Kanisa limemtangaza kuwa Mtakatifu.
Na tena si kila mtakatifu ameandikwa kwenye orodha ya watakatifu. Ndio kusema
kuwa wapo watakatifu wengi mno ambao hawajaandikwa kwenye kitabu cha watakatifu
na tena wapo watakatifu wengi mno ambao hawajatangazwa kuwa ni watakatifu.
Kwa msingi huo basi, Kumbuka
kwamba tarehe Mosi mwezi Novemba kila mwaka Kanisa huadhimisha Sherehe kwa
heshima ya Watakatifu wote. Kwa nini Kanisa limeweka siku hii ya pekee? Kanisa
limeweka siku hii ya pekee kuwakumbuka Watakatifu wote pamoja, kwa vile
linatambua kuwa idadi ya watakatifu katika Kanisa ni kubwa sana (rej.Ufu
7:9-12). Siku za mwaka hazitoshi kabisa kuwaheshimu Watakatifu wote mmoja
mmoja.
Tena hatuwezi kujua orodha kamili ya majina yao.
Kwa hiyo Kanisa limeweka siku ya pekee kwa ajili ya kuwakumbuka wote kwa
pamoja.
Watakatifu hawa tunaowakumbuka
kila 1/11 kila mwaka walikuwa binadamu kama sisi yaani walikuwepo; matajiri,
masikini, wanaume, wanawake, watoto, Wazungu, Waafrika nk. (rej. Ufu 7:9).
Watakatifu hawa walitambua kuwa, sababu ya
mtu kuumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ni kwamba yeye ni mali
ya Mungu na kwamba wito wa
kwanza wa kila mtu ni kuishi
kitakatifu kama Baba yetu wa
mbinguni alivyo Mtakatifu.
Tarehe au siku ambayo Kanisa hukumbuka watakatifu inamaanisha
nini, je, ni Kifo cha mtakatifu au kupewa utakatifu?
Kwa
kawaida Kanisa lina mazoea ya kuadhimisha sikukuu ya kila mtakatifu siku ya
kufa kwake kwa kuwa hiyo ndiyo siku ya kuingia kwake mbinguni yaani kuzaliwa
kwake katika umilele. Hata hivyo iwapo siku ya kufa mtakatifu husika
haijulikani, maadhimisho ya mtakatifu huyo hupangwa siku iliyo na uhusiano wa
pekee naye, kwa mfano, kama mtakatifu husika alikuwa ni padre basi anaweza
akakumbukwa siku aliyopewa Daraja Takatifu, au siku maiti ya mtakatifu husika
ilipogunduliwa au kuhamishwa.
Kazi za watakatifu ni nini?
Watakatifu kazi
yao ni kuomba kwa ajili yetu mbele ya Mungu, wakimtolea mastahili waliyokuwa
wameyapata duniani kwa njia ya mshenga mmoja wa Mungu na watu, Yesu Kristo. Tena,
kwa maisha yao wamekuwa kielelezo kinachotuletea mafundisho mengi kwa manufaa
ya roho zetu. Kwetu sisi sote tulioko hapa duniani tunataka umoja wa kanisa
lote uimarishwe kwa zoezi la mapendo ya kidugu. kwani kama ushirika kati ya Wakristo
duniani unavyotusogeza karibu zaidi na Kristo ndivyo umoja pamoja na watakatifu
unavyotuunganisha na Kristo.
Kwa nini mababu zetu wa kwanza ambao
waliishi vizuri hapa duniani kama akina Ibrahimu na Musa hawajatangazwa
watakatifu?
Ibrahimu aliye baba wa imani na Musa ni
watakatifu hao. Yapo baadhi ya maandishi ya Kikatoliki yanayothibitisha ukweli
huo wa kwamba Ibrahimu aliye baba wa imani na Musa ni Watakatifu. Ninakusihi
usome kitabu cha TUMSIFU MUNGU chuo cha sala na nyimbo katika ukurasa wa 450,
utapata pale orodha ya Watakatifu wote akiwemo Ibrahimu aliye baba wa imani na
Musa. Hapo ndipo ilipotolewa orodha ya Watakatifu wa Agano la Kale wakiwemo
mababu na manabii. Ni hapo utayakuta majina ya kama vile Mtakatifu Ibrahimu,
Mtakatifu Musa, Mtakatifu Eliya, Watakatifu mababu wa kale na manabii n.k
Tofauti inayojitokeza kati ya
Watakatifu hao wa Agano la Kale na wale wa Agano Jipya ni kutokana na historia
ya kutangaza watakatifu kama nilivyosema hapo awali kuwa, mwanzoni wafiadini
walipewa mara moja heshima ya pekee kwa sababu walikuwa wameishuhudia imani yao
kwa Kristo. Ndipo basi kuanzia karne takribani ya nne hivi wale ambao hawakuwa
wafiadini, nao walianza kupewa heshima kama hiyo hiyo. Hawa walikuwa ni
mashujaa waliovumilia maisha magumu na yenye taabu, kama vile wakaa pweke, wamonaki,
maaskofu na wale waliojihusisha na kutatua mafundisho rasmi ya dini yetu.
Hatimaye kuanzia karne ya kumi na tatu, akawa ni Papa peke yake ndiye aliyekuwa na uwezo wa kumtangaza mtu
kuwa mtakatifu.
Kwa hivi unaona haya yote yametokea
wakati wa Agano Jipya na si Agano la Kale. Lakini hata hivyo Kanisa
linawatambua mababu hao kuwa ni Watakatifu kutokana na maisha yao mzuri
waliyoyaishi pindi walipokuwa hapa duniani.
Je, Masalia ya watakatifu altareni si ushirikina?
Masalia ni mabaki ya mwili au vitu
vilivyotumika na mtakatifu fulani wakati wa uhai wake hapa duniani. Masalia
hayo huitwa matakatifu kwa vile yule aliyeyatumia au yaliyetokana na yeye sasa
ni mtakatifu. Hivyo Wakatoliki hutoa heshima kwa masalia hayo ya mtakatifu husika.
Kanisa katoliki limeyagawanya masalia
katika ngazi tatu: ngazi ya kwanza,
ni sehemu ya mwili, mfano mifupa; Ngazi
ya pili ni vitu alivyovitumia, mfano msalaba, vitabu, rozari; na ngazi ya tatu ni nguo zake alizotumia.
Hivyo masalia sio ushirikina. Tuelewe
kwamba, ushirikina ni imani juu ya
mtu au vitu fulani ambavyo husadikiwa kuwa na nguvu ya pekee ya kuleta au
kutenda jambo fulani zuri au baya, lisiloelezeka kiakili na hata kisayansi
pasipo kumshusha Mungu. Nguvu hizo zilikuwepo zamani, lakini Mungu alizikataza
kwa sababu ya kuziamini mno na kumwacha yeye. (rej. 2Sam 28:3; Wal 19: 31).
Mfano wa vitu vya kishirikina ni pamoja na hirizi, mizimu na ndoto za usiku.
Tangu zama za kale masalia
yaliheshimiwa na kuhifadhiwa vizuri. Babu zetu waliamini kwamba Mungu
huwatembelea kupitia masalia ya watu walioishi vizuri na ambao sasa ni
watakatifu, walijiona kama bado wameunganika kabisa na ndugu zao, na ndio maana
walipokuwa wakihama, waliondoka na masalia ya ndugu zao (rej. Kut 13:19, Mw 50:
25).
Kuanzia karne ya nne, mtindo wa
kuyahamisha masalia ya watakatifu kutoka makaburini au shehemu zile walipoishi,
kwenda makanisani ulianza na kushamiri sehemu nyingi duniani. Pale miujiza
ilipotendeka na kujulikana kutokana na masalia ya watakatifu, watu walifika
sehemu husika na kuomba kiasi cha masalia yake ili wayapeleke katika makanisa
yao. Na hapo ndipo ulipokuwa mwanzo wa kuweka masalia kanisani na baadaye kwa
namna ya pekee kabisa altareni.
Je, wakatoliki wanayaabudu masalia wanayoyaweka altareni?
Wakatoliki tunayaheshimu masalia ya
watakatifu; hatuyaabudu wala hatuyatumii kishirikina, bali sisi tunamwabudu
Mungu wetu mmoja katika nafsi zake tatu. Maisha ya mtakatifu husika ambaye
masalia yake yapo altareni, tunatagemea yawe ni changamoto kwetu sisi tupate
kutamani, kuhamasika na kuiga ili nasi
siku moja tuweze kuifikia hatua hiyo ya utakatifu. Mifano ya watakatifu hao
itufanye sisi kuimarika zaidi na kuwa wavumilivu kwa magumu na shida tunazozipata
kutokana na imani yao. Hivyo kwa maisha ya watakatifu sisi tunapata mbinu za
kuishi kadiri ya mapenzi ya Mungu.
Kumheshimu mtakatifu ni kumwomba
atuombee kwa Mungu, vilevile kuwaheshimu watakatifu ni kumheshimu Mungu
aliyewafanya wawe watakatifu. Na hivyo basi, kuheshimu masalia ni kumheshimu
mtakatifu husika na kwa upande mwingine ni kumuheshimu Mungu.
Masalia ya watakatifu huwekwa altareni
kwasababu: kwanza, altare ipo chini
ya ulinzi na uangalizi mkubwa na tena mtakatifu. Pili, altare ni takatifu, hivyo masalia lazima yawekwe mahali
patakatifu; na tatu, altare ni
mahali ambapo fumbo la Bwana wetu Yesu Kristo kujitoa sadaka kwa wokovu wa
ulimwengu linafanyika kila Misa inapoadhimishwa. Hivyo kuwekwa altareni kwa
masalia ya watakatifu hakuna uhusiano wowote na maswala ya kishirikina, bali
kwa maombezi ya mtakatifu husika na sadaka ya misa takatifu, waamini wapate
wokovu hapo baadaye.
Hitimisho
Kwa kuhitimisha tukumbuke kuwa watakatifu
walikuwa binadamu kama sisi, walipigana vita dhidi ya tamaa za mwili, majivuno,
mali, anasa, uzembe, uvivu na wivu, na kama haitoshi walifaulu kuwashinda maadui
hao wote wakiitumaini neema ya Mungu. Swali la kujiuliza mimi na wewe
ni kuwa tunashindanaje na vita dhidi ya maovu ambayo inadumu kwa muda mchache
tu hapa duniani? Tunajiandaaje kuipokea taji ya Utakatifu baada ya kifo chetu
kwa maandalizi tunayoyafanya?
Bila shaka hatuna budi kuwaomba
watakatifu ambao ni marafiki wa karibu wa Mungu. Mungu atawapa chochote kile
watakachoomba kwa ajili yetu. Tukumbuke kuwa wao wanatupenda sisi na wanatamani
sana nasi tupate kuokoka kama walivyo wao. Hivyo basi ikiwa sasa tunahangaishwa
na kusumbuliwa na vishawishi mbalimbali tusikate tama, hatuna budi kuinua mioyo
yetu juu na kuzitazama mbingu kwa jinsi zinavyopendeza.
Pd.
Dunstan Christantus Haule
Salesians
of Don Bosco