Tuesday, 4 April 2017

WATAKATIFU
UFAHAMU JUU YA WATAKATIFU
1.     Jinsi ya upatikanaji wa mmoja kuitwa Mtakatifu.
Maana ya neno  Mtakatifu
Katika Agano la Kale Mungu pekeyake aliitwa Mtakatifu (rej. Isaya 6:3). Pili neno Mtakatifu katika Agano la Kale lilitumika pia kwa wale waliowekwa wakfu kwa ajili ya utumishi wa Mungu (rej. Law 17:1).
Tukija katika Agano Jipya, Mtakatifu ni neno lenye asili ya lugha ya Kigiriki  “hagios” linalotumika katika Maandiko Matakatifu  hasa Agano Jipya kuwaonesha wafuasi wa Yesu. Wote wale waliosadiki na kubatizwa walijiunga na “ukoo mteule, makuhani wa Mfalme, taifa takatifu na watu wake Mungu mwenyewe”(1Petro 2:9). Mtakatifu ni neno pia linalowaelezea waamini walioishi kabla ya  wakati wa Yesu (Mathayo 27:52). Pia neno hili linatumika kwa wale walioingia katika Agano  Jipya na Yesu Kristo (Wafilipi 1:1). Mtakatifu kwa upande mwingine  ni kama jina mbadala  la  waamini  Wakristo wa Kanisa la mwanzo. Kwa mfano, Mtume Paulo alipenda kuwaita “watakatifu” wale wote aliokuwa akiwaandikia. Warumi 1:7,  Waefeso 1:1, 1Kor 1:2, 2Wakorintho 1:1.

Kupanuka kwa dhana ya Mtakatifu
Mtakatifu ni mtu yule aliyeko mbinguni ambaye anawaombea watu na Kanisa lililoko duniani wapate mahitaji yao. Mtu huyo anakuwa ametuzwa heshima na umati mkubwa wa watu na ametambuliwa na kanisa. Aidha,watakatifu ni kusanyiko kubwa sana la wazaliwa wa kwanza wa Mungu ambao majina yao yameandikwa mbinguni. Hizo ni roho za watu waadilifu waliofanywa kuwa watakatifu ambao wamejenga kusanyiko kubwa sana la watu hai ambao wamejitakatifuza kwa damu ya Yesu Kristo na kwa neema yake, katika kufuata nyayo zake na wakawa wametekeleza kazi inayompendeza Baba. Miongoni mwao wakiwa mashahidi ambao wamekuwa daima chemchemi  na asili ya kujifanya upya katika nyakati zilizokuwa ngumu  zaidi, ya historia ya kanisa.
Mashahidi ndio wale waliokubali kifodini kuliko kuachilia imani yao kwa Mungu. Hawa ni mashahidi wa Mungu. Kwa hiyo wote hao wakiwa wameungana kabisa pamoja na Kristo wanashiriki kulijenga kanisa kwa uthabiti zaidi katika utakatifu. Hapa ndipo tunapomkumbuka kwa namna ya pekee kabisa Stefano ambaye ndiye anayetajwa kama shahidi wa kwanza (Mdo 7: 52-60).

Nani anayerudisha jina toka mbinguni kuwa mtu fulani ni Mtakatifu?
Ni kwa njia ya ufunuo ambao Kanisa huupata kutoka kwa Mungu. Mungu anapotupa ufunuo wake kimsingi anakuwa anajibu yale maombi ambayo sisi binadamu tulioishi na mtu husika tunakuwa tuliyatuma kwake. Kwa kifupi basi hiyo shughuli nzima inafanywa na Mungu mwenyewe kupitia Kanisa lake na kwa namna ya pekee viongozi wa Kanisa akiwemo baba Mtakatifu.
Historia ya kumtangaza mtu kuwa mtakatifu
Jambo hili linayo historia yake. Katika historia ya kanisa hapo mwanzo wafiadini walipewa mara moja heshima ya pekee kwa sababu walikuwa wameishuhudia imani yao kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Mtume Peto na Paulo wanatoa ushuhuda huo baada ya kufa kifo dini kati ya mwaka 64 hadi 67 baada ya Kristo. Ndipo basi kuanzia karne takribani ya nne hivi wale ambao hawakuwa wafiadini, nao walianza kupewa heshima kama hiyo hiyo. Hawa walikuwa ni mashujaa waliovumilia maisha magumu na yenye taabu, kama vile wakaa pweke, wamonaki, maaskofu na wale waliojihusisha na kutatua mafundisho rasmi ya dini yetu.
Ndipo basi baadaye, majina ya watakatifu hao wake kwa waume, yaliorodheshwa na hivi kila askofu alikuwa na orodha ya watakatifu waliokufa katika jimbo lake. Mambo yaliendelea hivyo mpaka katika karne ya kumi, ambapo Papa Yohane wa Kumi na tano alianza kuyachunguza yeye mwenyewe maisha ya mkristo aliyekuwa ameishi kishujaa katika fadhila kabla ya kuliandika jina lake katika orodha ya watakatifu. Tangu hapo uchunguzi ukazidi kufanyika kwa uangalifu zaidi. Hatimaye kuanzia karne ya kumi na tatu, akawa ni Papa peke yake  ndiye aliyekuwa na uwezo wa kumtangaza mtu kuwa mtakatifu.


2.  Hatua zinazofuatwa katika kumtangaza mtu kuwa Mtakatifu
Tangazo la mtu fulani kuwa mtakatifu ni lazima lipitie hatua tatu muhimu ambapo bila hizo mtu hawezi kutangazwa kuwa mtakatifu. Ikumbukwe kuwa hatua hizo hupitiwa baada ya kuwa mtu amekufa na si wakati akiwa hai.

Hatua ya kwanza ni ile ya mtumishi wa Mungu.
Hii ni hatua ya kupeleka jina la mtu huyo mnayetaka atangazwe kuwa mtakatifu kwenye Idara maalumu inayoshughulikia utangazaji wa wenye heri na watakatifu, Idara hiyo inayo makao yake makuu huko Roma. Lengo la kupeleka jina hilo ni kutaka kuchunguza maisha ya mtu huyo kwa ukaribu zaidi. Uchunguzi huo hufanywa kwa kuhusisha maoni ya wananchi wote kwani mtu huyo atadaiwa kuwa aliishi vema sio tu na Wakatoliki au Wakristo bali na wananchi wote au jamii nzima ya watu waliokuwa wakimzunguka.
Hii ni shughuli inayochukua miaka mingi kidogo kwani huhitajika mashahidi waliomjua Mkristo huyo ili waweze kuhakikisha kabisa tena kwa mifano ushujaa wake. Shughuli hii husimamiwa na askofu wa jimbo alimokuwa akiishi Mkristo huyo. Ripoti hiyo iliyotumwa huko Roma huchunguzwa kwa makini na hata kutaka kujua kama kuna miujiza yeyote ambayo imefanyika kupitia maombezi yake mtu huyo. Ndipo basi kama wakuu hao wa Idara wakiona kuwa hayo yote yamethibitishwa bila ya shaka yeyote, hapo ruhusa rasmi hutolewa ya kumwita Mkristo huyo “Mtumishi wa Mungu”. Na hivyo ndivyo inavyokamilika hatua hiyo ya kwanza.

Hatua ya pili ni ile ya Mwenyeheri:
 Ni baada ya miaka kadhaa hatua hii ya pili huweza kuidhinishwa. Hii ni baada ya kurudia upya mambo yote yaliyokwishafanywa katika hatua ya kwanza yaani, mashahidi wanahojiwa ambao wanaweza kuthibitisha kinaganaga, na kama kwa maombezi ya Mtumishi wa Mungu, sala zilisikilizwa na miujiza ilitendeka; aidha, watu wengine huhojiwa tena ili waweze kuthibitisha jinsi Mtumishi wa Mungu alivyoishi kifadhila kwa ushujaa mkubwa. Kama haitoshi ushahidi huo na maelezo hayo yote lazima yaandikwe hata kiasi kinachofikia maelfu na maelfu ya kurasa. Hapo sasa ndipo kamati kuu huundwa na wahusika wa kamati huchaguliwa na Papa mwenyewe ili kuweza kufanya majadiliano ya kina sana juu ya fadhila na miujiza ya Mtumishi huyo wa Mungu.
Mwisho wa yote ni juu ya Papa mwenyewe baada ya kuyasoma hayo yote na kusali sana tena sana ili kuyajua mapenzi ya Mungu, kuamua kama anaweza kuikubali hatua ya pili au hapana. Kama ndivyo basi huyo, Mtumishi wa Mungu, hutangazwa kuwa “Mwenye Heri”.

Hatua ya tatu na ya mwisho ni kutangazwa mtakatifu. Kisha kutangazwa kuwa Mwenye Heri Kanisa na wanakanisa wote huombwa kusali kwa kumwomba huyo mwenye heri miujiza itendeke kwa jina lake. Hapa Kanisa hutumia haki ya binadamu ya kumuuliza Mungu kitu na kusuburi jibu.
Hii ni haki ambayo binadamu anakuwa nayo ilimradi tu hana nia ya kumjaribu Mungu. Muujiza wowote unaofanyika kwa jina la Mwenye Heri huyo huripotiwa kwenye Idara husika, lakini kila tukio linalodaiwa kuwa ni muujiza huchunguzwa tena na tena kwa ukamilifu kama kweli ni muujiza.
Ni dhahiri kwamba kazi hii huchukua miaka mingi sana kwani mikutano mingi hufanyika tena na tena, na majadiliano huwa ni mengi na watu wengi sana huhojiwa kuhusiana na suala hili.  Ni ukweli kuwa Kanisa huwa ni gumu katika kuipokea miujiza, kusudi  lisifanye makosa ya kutangaza tukio fulani kuwa ni muujiza wakati sio. Kwa kifupi Kanisa halitaki kujutia au kutangua kitu kilichotangazwa tayari.
Ndipo basi, miujiza saba ikitokea kwa jina la Mwenyeheri husika na kukubalika na Kanisa, Kanisa hujua kwamba Mungu amewabainishia kwamba mtu husika amefika katika makao matukufu ya Mungu mwenyewe. Hata hivyo mwenye kutoa uamuzi wa mwisho ni Papa mwenyewe ambaye, kwa mara nyingine anasali sana tena na tena ili apate kuyajua mapenzi ya Mungu katika jambo hilo. Kama baada ya shughuli hizo zote anaamua kuendelea, bila kipingamizi, basi hapo ndipo Papa katika Ibada maalumu humtangaza Mwenyeheri huyo kuwa Mtakatifu. Hivyo ndivyo zinavyokamilika hatua tatu za mtu kutangazwa kuwa Mtakatifu.








3.      Kuna utofauti gani kati ya utakatifu na wokovu?
4.      Ni vigezo vipi vinavyomfanya mtu aitwe mtakatifu?
5.      Juu ya Baba Mtakatifu
                                I.            Je, baba Mtakatifu ni Mtakatifu?
                              II.            Kuna utofauti gani kati ya utakatifu wa baba Mtakatifu na utakatifu wa watakatifu ambao kanisa huwakumbuka kila siku na kuadhimisha misa kwa heshima yao?
                            III.            Kuna umuhimu gani wa kukiita kiti cha baba Mtakatifu kitakatifu wakati yeye si mtakatifu?
                            IV.            Je, kuna watakatifu walio hai?
                              V.            Kwa nini Kanisa kuwakumbuka watakatifu wachache tena kujirudia mwaka hadi mwaka, hakuna walioishi kitakatifu zaidi ya hao?
                            VI.            Tarehe au siku ambayo Kanisa hukumbuka watakatifu inamaanisha nini? Kifo cha mtakatifu au kupewa utakatifu?
                          VII.            Kazi ya watakatifu ni nini?
6.      Kwa nini mababu zetu wa kwanza ambao waliishi vizuri hapa duniani kama akina Ibrahimu na Musa hawajatangazwa watakatifu?
7.      Juu ya Masalia ya watakatifu
                                I.            Je, ni halali masalia ya watakatifu kuwekwa altareni?
                              II.            Je, masalia ya watakatifu altareni si ushirikina?
                            III.            Kwa nini Wakatoliki wanayaabudu masalia yanayowekwa altareni?


Tofauti  kati ya utakatifu na wokovu?
Tofauti iliyopo kati ya utakatifu na wokovu ni ndogo sana, nayo ni hii kuwa mtu hawezi kutangazwa mtakatifu kama kwanza hajaokoka.
Hii ni kusema kuwa, baada ya kuwa mtu ameokoka yaani baada ya kifo chake na kupewa tunu na Mwenyezi Mungu ndipo hapo kanisa kwa kuangaziwa na Mungu huanza mchakato wa kumtangaza mtu husika kuwa Mtakatifu. Kwa maelezo hayo basi bado tunabaki palepale kuwa watakaookoka watakuwa ni wengi na pengine sio wote watakaotangazwa kuwa Watakatifu.
Kila aliye Mtakatifu ni lazima awe kwanza ameokoka lakini haya yote yanatokea baada ya kifo chake na sio kabla. Ni ukweli pia kuwa miongoni mwa watakaookoka ndio watakaotambuliwa kuwa ni Watakatifu. Kila atakayeokoka ni Mtakatifu ingawa anaweza kuwa ametangazwa kuwa Mtakatifu au hajatangazwa kuwa Mtakatifu.
Hata hivyo kwa ujumla maneno haya mawili yaani wokovu na utakatifu, hayapingani kwa yenyewe kwani yote yanamaanisha tunu, thawabu au heko ambayo mmoja anatunukiwa na Mungu baada ya kuwa aliishi vizuri pindi alipokuwa hapa duniani.
Ni vigezo vipi vinavyomfanya mtu aitwe Mtakatifu
Vigezo vya mmoja kutangazwa kuwa Mtakatifu ni kuishi vema hapa duniani, kufa vema na hatimaye kutunukiwa thawabu hiyo kubwa kabisa na Mungu mwenyewe. Kila mmoja anayo nafasi ya kuwa Mtakatifu hapo baadaye kwani nafasi hiyo haijatengwa kwa ajili ya mapapa tu, maaskofu, mapadre, masista n.k, la hasha nafasi hiyo ni ya kila mmoja ilimradi anaishi vema hapa duniani. Ndio maana ukisoma katika litania ya watakatifu wote utapata watakatifu mapapa, maaskofu, manabii, mapadre, watawa, walei na wengine chungu mzima.
Hapa Mwenyeheri Yohane wa XXIII atakayetangazwa kuwa Mtakatifu hapo kesho alikuwa na msemo mmoja kuwa “Inawezekana kuwa Mtakatifu wakati wa kushika fimbo ya askofu, lakini vile vile inawezekana kuwa Mtakatifu wakati wa kushika mkononi ufagio”.
Ndipo sasa ukienda mbali zaidi katika suala hili hili utagundua kuwa sio Wakristo tu ndio wanaoweza kuwa Watakatifu bali ni hata Waislamu, Wabudha, Wapagani na wote ambao hawatakuwa wamelipata neno la Mungu yaani kufikiwa na Kristo. Hii ni kwa sababu kila mtu atahukumiwa kadiri ya dhamiri yake, yaani kadiri mtu huyo alivyoisikiliza dhamiri hiyo. Mtume Paulo anatuhabarisha hayo anaposema kuwa “kuisikiliza dhamiri ni kumsikiliza Kristo mwenyewe” haya yanapatikana katika Rum 2:15-18 na 2Tim 4:1-4.
1.      Maelezo juu ya Baba Mtakatifu na utakatifu wake. Mfano halisia wa hayati baba Mtakatifu Yohana Paulo II ambaye Kanisa limemtangaza rasmi kuwa mtakatifu baada ya kifo chake, hata hivyo kutangazwa huko kumepitia hatua zote za kutangazwa mtakatifu.
 Tufahamu kuwa,Tunatumia neno mtakatifu tumtajapo Papa au kiongozi wetu mkuu kwa mfano Baba Mtakatifu Benedikto wa XVI, Baba Mtakatifu Fransis n.k kwa sababu ya kazi anayoisimamia au aliyokuwa akiisimamia, na si utakatifu wake yeye binafsi.
Hapa naomba nieleze japo kwa kifupi, kuhusu Baba Mtakatifu au Papa ni nani, sawia na mamlaka yake katika Kanisa Katoliki.  Papa ni wakili wa Yesu Kristo, Halifa wa Mtume Petro, Mkuu wa Kanisa Katoliki, Askofu wa jimbo la Roma. Zaidi ya hapo Baba Mtakatifu ni Rais wa Nchi ndogo ya Vatikani.
 Mintarafu madaraka ya Baba Mtakatifu, kwa jina lile la “Mwandamizi wa Petro” madaraka ya Baba Mtakatifu yachukuliwa kuwa yatoka kwa Mtume Petro aliyewekwa na Yesu mwenyewe kuwa “mwamba juu yake Kanisa lilijengwa” Nami nakuambia: Wewe ndiwe Petro na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu, wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni, na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni (rej. Mt 16:18-19; Lk 22:31-32).
Aidha ni Petro aliyepewa jukumu la kuwachunga na kuwalisha Kondoo wa Yesu “… Yesu akamwambia Simoni Petro, Je, Simoni wa Yohane, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia, Naam, Bwana wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha kondoo wangu. Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohane, wanipenda?
Akamwambia, ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu. Akamwambia mara ya tatu, ‘Simoni wa Yohane, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, ‘wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo wangu” (rej. Yn 21:15-17).

Maana ya fundisho la Yesu ni wazi. Hapa kondoo ni wale wote watakao mwamini au wafuasi wa Yesu Kristo, na hivi maana yake ni kwamba, Mtume Petro aliwekwa kuongoza na kutawala waamini na wachungaji wao. Huo ndiyo wajibu wa kichungaji aliokabidhiwa Mtume Petro na Yesu Kristo, ndiyo maana akakabidhiwa na ufunguo wa mamlaka ya kufunga na kufungua ya duniani naya mbinguni (rej. Mt 16:19). Wajibu huo wa kichungaji wa Mtume Petro ndiyo kwa sasa unaendelezwa na Baba Mtakatifu. Hivyo basi, Papa ni jaji mkuu wa mambo yote ya imani na maadili katika kutamka na kutumia mamlaka yake yasiyopingika.

Lakini wapo watu wanaopotosha kwa kusema kwamba ‘mwamba’ ule ni jiwe dogo. Lakini sisi twasema kwamba si hivyo kwa kuwa “Petros” kwa lugha ya Kigiriki, “Petra” kwa lugha ya Kilatini na “Kefas” kwa lugha ya Kiebrania, kila mara maana yake ni mwamba mkubwa.
Pia, wapo wanaosema kwamba ahadi hiyo ya Yesu ilikuwa kwa Simoni Petro tu, wala haiwahusu wale waliomfuata Petro. Lakini maelezo Katoliki yasema kwamba hiyo haiwezekani kabisa: mwamba wa Kanisa lazima uwe mwamba wa kudumu. Yaani katika maana ya kurithishwa kwa waandamizi wengine watakaofuata baada ya kifo cha Petro. Tukisema kwamba kauli ya Yesu ilimlenga Petro peke yake basi ingebidi huyo Petro asife au Kanisa nalo life baada ya kifo chake.
Sisi tunaamini kwamba Kanisa Katoliki ni la kweli kwa sababu limejengwa juu ya Mwamba wa Upapa na linakubali Uchungaji wa upapa. Kanisa Katoliki lipo tangu Papa wa kwanza, yaani Petro. Katika karne ya kwanza wapo mahalifa wake, yaani Linus, Anakleti, Klement na Evaristi. Zaidi, tunayo orodha ya mapapa wote mpaka Fransis aliye Papa kwa sasa.
Tangu halifa wa kwanza wa Bwana wetu Yesu Kristo, yaani Mtume Petro, hadi leo hii tunao Mapapa 266, ikiwa ni pamoja na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa XVI ambaye ni wa 265, na Papa anayeliongoza Kanisa Katoliki kwa sasa ambaye ni Baba Mtakatifu Fransis yeye ni wa 266.
 Yesu alimchagua Simoni Petro kuwa kiongozi mkuu na wa kwanza wa Kanisa lake. Petro aliliongoza Kanisa tangu mwaka 33 baada ya kupaa kwa Yesu mbinguni mpaka mwaka 67 alipokufa kifo dini. Mtume Petro, kufuatana na ushahidi dhahiri alikufa Roma, na kaburi lake liligunduliwa chini ya Altare Kuu ya Kanisa la Mtakatifu Petro huko Roma.
Tangu hapo utumishi huo (kiti hicho) umekuwa ukirithiwa bila kukatishwa mpaka leo hii, ambapo tunaye Papa wa 266 tangu wakati wa Petro. Tukisema kwamba kauli ya Yesu ilimlenga Petro peke yake basi ingebidi huyo Petro asife au Kanisa nalo life baada ya kifo chake. Lengo la Yesu lilikuwa ni kutunza umoja wa Kanisa lake, hivyo Papa ni ishara ya umoja huo. Tukumbuke kwamba bila ya Papa hakuna ukweli wala umoja. Matokeo ya kumkana ni madhehebu maelfu na maelfu ya Kikristo yaliyojitokeza katika historia ya Kanisa.
Huo ndio ufupisho kuhusu Baba Mtakatifu na wadhifa wake katika Kanisa Katoliki.


Je, papa au baba Mtakatifu ni Mtakatifu na kwa nini tunakiita kiti cha papa kitakatifu?
Kumbe basi tunaposema Papa au baba Mtakatifu hatumaanishi kuwa yeye ni Mtakatifu la hasha bali kilichokitakatifu ni kiti anachokikalia huyo baba Mtakatifu. Kiti hicho ni Kitakatifu kwa sababu Yesu Kristo mwenyewe aliye si tu mtakatifu bali ni utakatifu wenyewe alimteua Petro Mtume wake kama Papa au baba Mtakatifu wa kwanza kukalia kiti hicho cha kuliongoza Kanisa.
Ndio kusema kuwa Papa anaitwa Baba Mtakatifu si kwa nafsi yake kama mwanadamu bali ni cheo na dhamana ya kazi yake kama mwakilishi wa Mungu katika Kanisa. Hivyo utakatifu wa Papa siyo hasa wa maisha yake binafsi bali ni wa kazi yake.
Kama kazi ya Kanisa zima ni kutakatifuza waamini basi huyo mwenye dhamana ya kusimamia kazi zote za kutakatifuza ni Mtakatifu. Anaweza akawa mtakatifu au asiwe mtakatifu hilo litategemea na neema za Mungu na bidii yake mwenyewe (rej. 1Kor 9: 26-27), lakini si kwamba ana tiketi ya kwenda mbinguni moja kwa moja. Ila vile vile anayo nafasi nzuri zaidi ya kuwa mtakatifu kwa vile ukaribu na Mungu anaokuwa nao.
Ni kwa sababu hiyo basi kati ya mapapa 264 waliokwishapita si wote waliotangazwa kuwa ni watakatifu bali ni wachache tu. Na hii ni kudhihirisha kuwa wapo mapapa wengine ambao wameshindwa kupewa tunu hii ya utakatifu na mwenyezi Mungu au wamepewa tunu hiyo lakini Kanisa bado haliwatambui kama ni watakatifu. Hivyo basi hakuna ukweli wowote kuwa kila atakayekuwa baba Mtakatifu ni lazima awe Mtakatifu. Vigezo na masharti ni muhimu kuzingatiwa katika hili na tena huwezi kuwa Mtakatifu kama hujapitia hatua zile tatu za kuwa Mtakatifu, yaani kutangazwa kama mtumishi wa Mungu, mwenyeheri na hatimaye kutangazwa rasmi kama Mtakatifu.
Hata hivyo kwa upande wa papa Yohane Paulo wa II, usijali kwani hatimaye Baba Mtakatifu huyu ametimiza vigezo na hivyo na hivyo Yohane Paulo wa Pili kuitwa Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili.

Kuna utofauti gani kati ya utakatifu wa baba Mtakatifu na utakatifu wa watakatifu ambao Kanisa huwakumbuka kila siku na kuadhimisha misa kwa heshima yao?
Kama tulivyoona kwamba, utakatifu wa baba mtakatifu si wa kwake yeye mwenyewe binafsi bali ni wa mambo anayoyasimamia. Kwa upande mwingine utakatifu wa watakatifu ambao mama Kanisa huadhimisha misa kwa heshima yao kwa mfano akina Mtakatifu Augustino akina Mtakatifu Katalina wa Siena, Mtakatifu Yohane Bosco, Dominiki Savio na wa wengine wengi ni utakatifu wao binafsi. Yaani niwatakatifu katika maana halisi ya utakatifu. Na hawa wapo mbinguni.
 Tukija kwa upande wa Baba Mtakatifu, kwa mfano sasa tunaye papa Fransis, tunamwita Baba Mtakatifu Fransis kutokana na dhamana anayoishikilia yaani ya kuliongoza Kanisa na wala si utakatifu wake yeye binafsi kwa kusema hivyo hatukatai kwamba yeye si au hawezi kuwa mtakatifu la hasha!
Tunachomaanisha kwamba naye lazima kwanza afe kisha kufa kama kuna ulazima wa kumtangaza mtakatifu ndipo naye afuate mchakato ule ule wa mmoja kutangazwa Mtakatifu.
Laiti tungewaita mapapa Mababa Watakatfu tukimaanisha utakatifu hao binafsi basi kusingekuwa na haja ya wao kufuata hatua hizo ambazo nimekwisha zitaja ili kuwatangaza. Kwa kifupi ni kwamba hatua za kumtangaza mmoja kuwa mtakatifu ni zilezile kwa watu wote haijalishi mhusika alikuwa papa au mwanajeshi au rais nk.
Ndipo basi katika mchakato kama huu wa mmoja kutangazwa kuwa Mtakatifu hakuna undugu au rushwa. Hakuna kusema labla kwa sababu mmoja alikuwa Papa basi apate upendeleo, haya ni kinyume na maadili ya Kanisa letu lenye sifa ya Utakatifu ndani yake. Mchakato huu mzima unahusisha sala kwa Mwenyezi Mungu na ndanimo hatutegemei kuona upendeleo, urafiki, undugu, urangi, ubara, ujinsia au ubaguzi wa aina yeyote ile. Ni Kanisa ndilo linalojulishwa na Mungu kwa ufunuo kwamba mtu fulani aliyeishi vizuri hapa duniani ameutafuta uzima wa milele kwa mafanikio, na hivi mtu huyo hanabudi kuwekwa kama mfano mbele ya wengine wanaoendelea kutafuta kwa mafanikio uzima wa milele.

Kuna umuhimu gani wa kukiita kiti cha baba Mtakatifu kitakatifu wakati yeye si mtakatifu?
Umuhimu wa kukiita kiti cha baba Mtakatifu kitakatifu, hata kama tunasema kuwa si kila anayekalia kiti hicho kitakatifu ni lazima awe Mtakatifu. Ninasema upo umuhimu kwa sababu yeye aliyempa Petro kiti hicho kwa mara ya kwanza, si tu ni Mtakatifu bali yeye ni utakatifu wenyewe.

Je, kuna watakatifu walio hai?
Hakuna Mtakatifu aliyehai ndugu yangu. Kama nilivyokuambia kuwa ili mmoja atangazwe kuwa Mtakatifu ni lazima apitie hatua tatu yaani kutangazwa kama mtumishi wa Mungu, Mwenyeheri na hatimaye kutangazwa rasmi kama mtakatifu, halafu basi hakuna hatua yeyote kati ya hizi ambayo mmoja anaweza kuipitia akiwa angali hai. Ni lazima kufa kwanza ndipo michakato mingine yote huweza kufuata. Ila kuna watu wengi wanaouishi utakatifu (maisha matakatifu) hapa duniani.
Mmoja anayetangazwa Mtakatifu hutangazwa sio kabla, bali ni baada ya kufa na maisha yake kuchunguzwa sana kama Maandiko Matakatifu yenyewe yanavyotushauri (rej. Ebr 13:7-9a). Hapa, waamini tunapewa ruhusa kuwakumbuka wale waliotutangulia katika imani kwa kuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao kusudi tuige imani yao kwa vile tunayepaswa kumtumikia ni Yesu Kristo ambaye ni yeye yule, jana, leo na hata milele. Kwa maana hii basi, jinsi walivyotumikia wenzetu inaweza kutufaa sisi pia ambao bado tunaishi hapa duniani. Hao hutangazwa watakatifu kama Biblia inavyosema baada ya kufa kwao kwani ndipo tabia yao halisi ya binadamu huwa imepita picha kamili (rej. YbS 11:27b-28).
Ndugu zangu, hata hivyo utakatifu si wito wa watu wachache, sisi sote tunaalikwa kuwa watakatifu. Na utakatifu wenyewe tunaanza kuutafuta hapa hapa duniani. Maana yake tungalibado hai. Isipokuwa, Kanisa pamoja na kutuhimiza kuuchuchumalia utakatifu uliowito wetu sisi sote halijawahi kamwe kumtangaza mtu ambaye bado yuko hai kuwa Mtakatifu. Kwa nini? Kwa sababu, hujafa hujaumbika!
 Ifahamike pia kuwa hata kuokoka hakuwezekani tunapokuwa duniani hapa. Ukweli ni kwamba kuokoka kadiri ya Maandiko Matakatifu kunatokea baada ya kuwa safari ya hapa duniani imekwisha yaani baada ya kifo na sio vinginevyo. Tunaweza kuona kwamba Biblia inataka kuonesha kuwa kuokoka halisi ni kilele cha wokovu wetu, ni kuurithi uzima wa milele, ni kumwona Mungu kama alivyo kama inavyosomeka katika Mdo 15:11; Rum 5:9-10; na Ebr 12:25.
Ikumbukwe kuwa kwa mtu kuniingilia mimi niliye Mkristo na tena Mkatoliki na kuniambia kuwa yanipasa kuokoka ni sawa na kukiona kibanzi kwenye jicho langu na kusahau gogo lililo kwenye jicho lake. Ni nani basi aliyeokoka hapa duniani? Bila shaka hakuna ila sote tunauelekea huo wokovu ambao unakamilika kwa hatua tatu yaani;
Mosi; ni hatua ya kubatizwa au kuzaliwa upya. Hatua ya pili ni ile ya kuyaishi maagano ya ubatizo yaani kuutafuta uzima wa milele kwa maisha ya kila siku. Hatua ya tatu ni ile ya kupokelewa mbinguni kama mshindi wa vita na kuvikwa taji ya ushindi yaani kupewa na Mungu uzima wenyewe.
Ninasema hivyo kwa makusudi mazima kwamba njiani mambo yanaweza kugeuka na kuwa vile ambavyo sisi hatukutegemea. Hapa ikumbukwe kuwa mambo yanaweza kuanza vema lakini mwisho wake ukawa ni mbaya au kinyume chake pia. Tukumbuke mfano mdogo tu ambao tunauweka kwa vipimo vya kibinadamu  huu ni ule wa Yuda, mtume wa Yesu Kristo na mweka hazina wa mitume na wafuasi wa Yesu aliyeanguka kwenye kishawishi cha mali akaishia kujinyonga na kupasuka tumbo (rej. Mdo 1:17-20). Je, kama mtume huyu angejigamba alipoishi hapa duniani na kujiita aliyeokoka ingekuwaje kuanguka dhambini, tena kwa nafasi nyeti kama ile aliyekuwanayo.Waswahili husema kwamba usitukane mamba kabla hujavuka mto. Maandiko Matakatifu pia yanatuambia wa kwanza anaweza kuwa wa mwisho na wa mwisho anaweza kuwa wa kwanza (rej. Mt 19:30, Mk 10:31, Lk 11:26) na ndipo tunapoaswa kwamba kwa aliyeanza safari ya kuutafuta uzima wa milele basi avumilie na yule atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokoka.
Kwa hivi hakuna anayeweza kuitwa Mtakatifu akiwa angali bado hai hapa duniani na wala hakuna anayeweza kuitwa aliyeokoka akiwa hapa duniani. Sisi sote tupo safarini kuuelekea huo utakatifu, kuuelekea huo wokovu, hivyo ni baada ya kifo ndipo mmoja anaweza kuwa Mtakatifu au aliyeokoka.

Kwa nini Kanisa huwakumbuka watakatifu wachache tena kujirudia mwaka hadi mwaka, hakuna walioishi kitakatifu zaidi ya hao
Itambulike kuwa dadi ya watakatifu tokea kuumbwa kwa ulimwengu ni wengi sana ila wale wanaotambuliwa na Kanisa ndio wachache. Hili linatokana na historia ya kutangazana watakatifu kama nilivyokueleza hapo awali. Nimeeleza kuwa katika historia ya kanisa hapo mwanzoni wafiadini walipewa mara moja heshima ya pekee kwa sababu walikuwa wameishuhudia imani yao kwa Bwana wetu Yesu Kristo wakati walipomfia. Walikuwa na hakika kabisa kwamba wafiadini hao walikuwa pamoja na Yesu mbinguni.  Ni kuanzia karne takribani ya nne hivi wale ambao hawakuwa wafiadini, nao walianza kupewa heshima kama hiyo hiyo.
Kumbe basi baadaye, majina ya watakatifu hao wake kwa waume, yaliorodheshwa na hivi kila askofu alikuwa na orodha ya watakatifu waliokufa katika jimbo lake. Mambo yaliendelea hivyo mpaka katika karne ya kumi, ambapo Papa Yohane wa Kumi na tano alianza kuyachunguza yeye mwenyewe maisha ya Mkristo aliyekuwa ameishi kishujaa katika fadhila kabla ya kuliandika jina lake katika orodha ya watakatifu. Tangu hapo uchunguzi ukazidi kufanyika kwa uangalifu zaidi. Hatimaye kuanzia karne ya kumi na tatu, akawa ni Papa peke yake  ndiye aliyekuwa na uwezo wa kumtangaza mtu kuwa mtakatifu.
Ni kutokana na historia hiyo, si kila aliyetunukiwa cheo cha utakatifu na Mungu Kanisa limemtangaza kuwa Mtakatifu. Na tena si kila mtakatifu ameandikwa kwenye orodha ya watakatifu. Ndio kusema kuwa wapo watakatifu wengi mno ambao hawajaandikwa kwenye kitabu cha watakatifu na tena wapo watakatifu wengi mno ambao hawajatangazwa kuwa ni watakatifu.
Kwa msingi huo basi, Kumbuka kwamba tarehe Mosi mwezi Novemba kila mwaka Kanisa huadhimisha Sherehe kwa heshima ya Watakatifu wote. Kwa nini Kanisa limeweka siku hii ya pekee? Kanisa limeweka siku hii ya pekee kuwakumbuka Watakatifu wote pamoja, kwa vile linatambua kuwa idadi ya watakatifu katika Kanisa ni kubwa sana (rej.Ufu 7:9-12). Siku za mwaka hazitoshi kabisa kuwaheshimu Watakatifu wote mmoja mmoja.
Tena  hatuwezi kujua orodha kamili ya majina yao. Kwa hiyo Kanisa limeweka siku ya pekee kwa ajili ya kuwakumbuka wote kwa pamoja.
Watakatifu hawa tunaowakumbuka kila 1/11 kila mwaka walikuwa binadamu kama sisi yaani walikuwepo; matajiri, masikini, wanaume, wanawake, watoto, Wazungu, Waafrika nk. (rej. Ufu 7:9). Watakatifu hawa walitambua kuwa, sababu ya  mtu kuumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ni  kwamba yeye ni  mali  ya Mungu na  kwamba  wito wa  kwanza wa  kila  mtu ni kuishi   kitakatifu kama  Baba yetu wa mbinguni alivyo Mtakatifu.

Tarehe au siku ambayo Kanisa hukumbuka watakatifu inamaanisha nini, je, ni Kifo cha mtakatifu au kupewa utakatifu?
Kwa kawaida Kanisa lina mazoea ya kuadhimisha sikukuu ya kila mtakatifu siku ya kufa kwake kwa kuwa hiyo ndiyo siku ya kuingia kwake mbinguni yaani kuzaliwa kwake katika umilele. Hata hivyo iwapo siku ya kufa mtakatifu husika haijulikani, maadhimisho ya mtakatifu huyo hupangwa siku iliyo na uhusiano wa pekee naye, kwa mfano, kama mtakatifu husika alikuwa ni padre basi anaweza akakumbukwa siku aliyopewa Daraja Takatifu, au siku maiti ya mtakatifu husika ilipogunduliwa au kuhamishwa.

Kazi za  watakatifu ni nini?
Watakatifu kazi yao ni kuomba kwa ajili yetu mbele ya Mungu, wakimtolea mastahili waliyokuwa wameyapata duniani kwa njia ya mshenga mmoja wa Mungu na watu, Yesu Kristo. Tena, kwa maisha yao wamekuwa kielelezo kinachotuletea mafundisho mengi kwa manufaa ya roho zetu. Kwetu sisi sote tulioko hapa duniani tunataka umoja wa kanisa lote uimarishwe kwa zoezi la mapendo ya kidugu. kwani kama ushirika kati ya Wakristo duniani unavyotusogeza karibu zaidi na Kristo ndivyo umoja pamoja na watakatifu unavyotuunganisha na Kristo.

Kwa nini mababu zetu wa kwanza ambao waliishi vizuri hapa duniani kama akina Ibrahimu na Musa hawajatangazwa watakatifu?  
 Ibrahimu aliye baba wa imani na Musa ni watakatifu hao. Yapo baadhi ya maandishi ya Kikatoliki yanayothibitisha ukweli huo wa kwamba Ibrahimu aliye baba wa imani na Musa ni Watakatifu. Ninakusihi usome kitabu cha TUMSIFU MUNGU chuo cha sala na nyimbo katika ukurasa wa 450, utapata pale orodha ya Watakatifu wote akiwemo Ibrahimu aliye baba wa imani na Musa. Hapo ndipo ilipotolewa orodha ya Watakatifu wa Agano la Kale wakiwemo mababu na manabii. Ni hapo utayakuta majina ya kama vile Mtakatifu Ibrahimu, Mtakatifu Musa, Mtakatifu Eliya, Watakatifu mababu wa kale na manabii n.k
Tofauti inayojitokeza kati ya Watakatifu hao wa Agano la Kale na wale wa Agano Jipya ni kutokana na historia ya kutangaza watakatifu kama nilivyosema hapo awali kuwa, mwanzoni wafiadini walipewa mara moja heshima ya pekee kwa sababu walikuwa wameishuhudia imani yao kwa Kristo. Ndipo basi kuanzia karne takribani ya nne hivi wale ambao hawakuwa wafiadini, nao walianza kupewa heshima kama hiyo hiyo. Hawa walikuwa ni mashujaa waliovumilia maisha magumu na yenye taabu, kama vile wakaa pweke, wamonaki, maaskofu na wale waliojihusisha na kutatua mafundisho rasmi ya dini yetu. Hatimaye kuanzia karne ya kumi na tatu, akawa ni Papa peke yake  ndiye aliyekuwa na uwezo wa kumtangaza mtu kuwa mtakatifu.
Kwa hivi unaona haya yote yametokea wakati wa Agano Jipya na si Agano la Kale. Lakini hata hivyo Kanisa linawatambua mababu hao kuwa ni Watakatifu kutokana na maisha yao mzuri waliyoyaishi pindi walipokuwa hapa duniani.

Je, Masalia ya watakatifu altareni si ushirikina?
Masalia ni mabaki ya mwili au vitu vilivyotumika na mtakatifu fulani wakati wa uhai wake hapa duniani. Masalia hayo huitwa matakatifu kwa vile yule aliyeyatumia au yaliyetokana na yeye sasa ni mtakatifu. Hivyo Wakatoliki hutoa heshima kwa masalia hayo ya  mtakatifu husika.
Kanisa katoliki limeyagawanya masalia katika ngazi tatu: ngazi ya kwanza, ni sehemu ya mwili, mfano mifupa; Ngazi ya pili ni vitu alivyovitumia, mfano msalaba, vitabu, rozari; na ngazi ya tatu ni nguo zake alizotumia.
Hivyo masalia sio ushirikina. Tuelewe kwamba, ushirikina ni imani juu ya mtu au vitu fulani ambavyo husadikiwa kuwa na nguvu ya pekee ya kuleta au kutenda jambo fulani zuri au baya, lisiloelezeka kiakili na hata kisayansi pasipo kumshusha Mungu. Nguvu hizo zilikuwepo zamani, lakini Mungu alizikataza kwa sababu ya kuziamini mno na kumwacha yeye. (rej. 2Sam 28:3; Wal 19: 31). Mfano wa vitu vya kishirikina ni pamoja na hirizi, mizimu na ndoto za usiku.
Tangu zama za kale masalia yaliheshimiwa na kuhifadhiwa vizuri. Babu zetu waliamini kwamba Mungu huwatembelea kupitia masalia ya watu walioishi vizuri na ambao sasa ni watakatifu, walijiona kama bado wameunganika kabisa na ndugu zao, na ndio maana walipokuwa wakihama, waliondoka na masalia ya ndugu zao (rej. Kut 13:19, Mw 50: 25).
Kuanzia karne ya nne, mtindo wa kuyahamisha masalia ya watakatifu kutoka makaburini au shehemu zile walipoishi, kwenda makanisani ulianza na kushamiri sehemu nyingi duniani. Pale miujiza ilipotendeka na kujulikana kutokana na masalia ya watakatifu, watu walifika sehemu husika na kuomba kiasi cha masalia yake ili wayapeleke katika makanisa yao. Na hapo ndipo ulipokuwa mwanzo wa kuweka masalia kanisani na baadaye kwa namna ya pekee kabisa altareni.

Je, wakatoliki wanayaabudu masalia wanayoyaweka altareni?
Wakatoliki tunayaheshimu masalia ya watakatifu; hatuyaabudu wala hatuyatumii kishirikina, bali sisi tunamwabudu Mungu wetu mmoja katika nafsi zake tatu. Maisha ya mtakatifu husika ambaye masalia yake yapo altareni, tunatagemea yawe ni changamoto kwetu sisi tupate kutamani,  kuhamasika na kuiga ili nasi siku moja tuweze kuifikia hatua hiyo ya utakatifu. Mifano ya watakatifu hao itufanye sisi kuimarika zaidi na kuwa wavumilivu kwa magumu na shida tunazozipata kutokana na imani yao. Hivyo kwa maisha ya watakatifu sisi tunapata mbinu za kuishi kadiri ya mapenzi ya Mungu.
Kumheshimu mtakatifu ni kumwomba atuombee kwa Mungu, vilevile kuwaheshimu watakatifu ni kumheshimu Mungu aliyewafanya wawe watakatifu. Na hivyo basi, kuheshimu masalia ni kumheshimu mtakatifu husika na kwa upande mwingine ni kumuheshimu Mungu.
Masalia ya watakatifu huwekwa altareni kwasababu: kwanza, altare ipo chini ya ulinzi na uangalizi mkubwa na tena mtakatifu. Pili, altare ni takatifu, hivyo masalia lazima yawekwe mahali patakatifu; na tatu, altare ni mahali ambapo fumbo la Bwana wetu Yesu Kristo kujitoa sadaka kwa wokovu wa ulimwengu linafanyika kila Misa inapoadhimishwa. Hivyo kuwekwa altareni kwa masalia ya watakatifu hakuna uhusiano wowote na maswala ya kishirikina, bali kwa maombezi ya mtakatifu husika na sadaka ya misa takatifu, waamini wapate wokovu hapo baadaye.

Hitimisho
Kwa kuhitimisha tukumbuke kuwa watakatifu walikuwa binadamu kama sisi, walipigana vita dhidi ya tamaa za mwili, majivuno, mali, anasa, uzembe, uvivu na wivu, na kama haitoshi walifaulu kuwashinda maadui hao wote wakiitumaini neema ya Mungu. Swali la kujiuliza mimi na wewe ni kuwa tunashindanaje na vita dhidi ya maovu ambayo inadumu kwa muda mchache tu hapa duniani? Tunajiandaaje kuipokea taji ya Utakatifu baada ya kifo chetu kwa maandalizi tunayoyafanya?
Bila shaka hatuna budi kuwaomba watakatifu ambao ni marafiki wa karibu wa Mungu. Mungu atawapa chochote kile watakachoomba kwa ajili yetu. Tukumbuke kuwa wao wanatupenda sisi na wanatamani sana nasi tupate kuokoka kama walivyo wao. Hivyo basi ikiwa sasa tunahangaishwa na kusumbuliwa na vishawishi mbalimbali tusikate tama, hatuna budi kuinua mioyo yetu juu na kuzitazama mbingu kwa jinsi zinavyopendeza.




Pd. Dunstan Christantus Haule
Salesians of Don Bosco



1 comment: