JIBU LA JUMLA KWA SWALI JUU SABATO
Baadhi ya maswali yaulizwayo:
Ø Kulingana na Maandiko Matakatifu Mungu anapaswa kuabudiwa siku ya Sabato.
Kwa nini Kanisa Katoliki husali siku ya kwanza ya juma? Kama kuna vifungu vya
Biblia vinavyohusu kusali siku ya kwanza ya juma naomba nipatiwe.
Ø Viongozi wa Kanisa Katoliki hawaoni kuwa Sabato ni Agano la milele na wala
siyo jumapili?
Ø Katika Maandiko Matakatifu Mungu anasema ikumbukwe siku ya sabato na kanisa
katoliki linasema shika kitakatifu siku ya Bwana yaani Jumapili, hamuoni kuwa
mnapingana na Mungu mkuu?
Ø Hamuoni kuwa kusali Jumapili ni amri ya binadamu na wala siyo ya Mungu?
Ø Yesu anasema tufundishe watu yale tu aliyofundisha, kama tusomavyo Mt. 28:19-20, 2Timotheo 3:16, Kumb. 4:2.
Inakuwaje mnafundisha kuwa Jumapili ni siku ya Sabato? Je, kufuatana na
Maandiko Jumapili ni siku ya ngapi? Je, Mungu alisema tusali Jumapili badala ya
Jumamosi? N.K.
Neno “sabato” hutokana na neno
la kiyahudi “shabbath” lenye maana
ya kukoma, kuacha au kupumzika kufanya kazi. Hii ndiyo maana ya msingi wa neno
sabato. Katika matumizi ya baadaye neno hili lilichukua maana ya siku ya saba
ya juma ambayo ilikuwa siku ya mapumziko. Hii ni maana ndogo tu ya neno sabato.
Kwa nini wayahudi walishika na wanaishika sabato. Wayahudi huishika sabato
kwa sababu tatu kama ndiyo msingi wa amri ya kupumzika:
Sababu ya kwanza ni kukumbuka kitendo cha kuondolewa toka utumwani Misri,
kama tusomavyo katika kitabu cha Kumbukumbu
la Torati 5:12-15 “Ishike siku ya
sabato uitakase-siku hiyo usifanye kazi yoyote-Nawe utakumbuka ya kuwa wewe
ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri-Mungu wako alikutoa huko kwa mkono wenye
nguvu- Kwa sababu hiyo Bwana Mungu wako, alikuamuru uishike sabato.”
Sababu ya pili ni kukumbuka siku alipopumzika Mungu baada ya kumaliza kazi
ya uumbaji; kama tusomavyo katika kitabu cha Kutoka 20:9-11 “Siku sita
fanya kazi lakini siku ya saba ni sabato ya Bwana-usifanye kazi yoyote, maana
kwa siku sita bwana alifanya mbingu na nchi, akastarehe siku ya saba.” Vile
vile tunaweza kusoma kitabu cha Mwanzo
2:3.
Sababu ya tatu na mwisho ni kwamba sabato ni alama ya
kwamba Mungu aliliteua taifa la Israeli kuwa mali yake. Kama tunavyosoma katika
kitabu cha Kutoka 13:13 “Hakika mtazishika sabato zangu, kwa kuwa ni
ishara kati ya mimi na ninyi katika vizazi vyenu vyote, ili mpate kujua ya kuwa
mimi ndimi Bwana niwatakasaye ninyi.”
Hizo ndizo sababu tatu za msingi ambazo huwasukuma wayahudi kuishika
sabato.
Sabato ilikuwa ni sikukuu ya kila juma kwa wayahudi wote.
Sasa tuangalie jinsi wayahudi
walivyoisherehekea sabato.
Sabato ilianza siku ya sita (yaani Ijumaa) jioni jua lilipozama. Kabla yake
watu walijiandaa kwa kuipamba nyumba, kutayarisha chakula kitakacholiwa siku ya
sabato, watu walivaa vizuri, na mama wa nyumba aliwasha mishumaa miwili ya
sabato. Walifanya hivi kwa sababu waliiheshimu sabato kama bibi harusi ambaye
inabidi apokelewe ki-sikukuu. Baada ya maandalizi, jioni ile ya Ijumaa wakati
wa kuzama jua, mtumishi wa sunagogi alipiga baragumu mara tatu kuashiria kuanza
kwa sabato. Jioni hiyo sabato ilisherehekewa katika sunagogi na nyumbani.
Basi jioni watu walikusanyika katika sunagogi kusali. Sala kwa nafasi hii
zilikuwa ni za kumshukuru na kumsifu Mungu aliyewapa watu siku ya sabato. Baada
ya sala walirudi nyumbani ambako walikula mlo wa sabato. Kabla ya mlo baba wa
nyumba alitamka sala ya sifa na baraka ijulikanayo kama “Kiddush”, kwa ajili ya
kuwabariki watoto na mama yao, na kumshukuru Mungu aliyewapa mkate na divai.
Kwa myahudi kula bila kubariki chakula ni wizi, ni kumwibia Mungu chakula (ni
sawa na kula takataka)- kwani vitu vyote ni mali ya Mungu. Wakati wa kula
waliweka vituo mbalimbali na kuimba nyimbo za kumsifu na kumshukuru Mungu. Siku
ya sabato yenyewe, asubuhi, ilifanyika ibada rasmi katika sunagogi au hekelu.
Kushika sabato:
Sheria za namna ya kuishika sabato zilikaziwa sana.Wayahudi walitakiwa
kuitumia sabato vema, siyo tu waliacha kufanya kazi bali pia hawakuruhusiwa
kufanya mipango au kuzungumzia kazi zijazo au zilizopita. Hiyo nayo ilihesabiwa
kuwa ni kazi. Haikuiruhusiwa kufanya kazi yoyote wala na mtumwa au mgeni wala
hata na mnyama. Mazungumzo yote yalitakiwa yawe ni mambo ya dini tu.
Kazi zilizokatazwa kufanyika siku ya sabato:
Kazi za wayahudi zilipangwa
katika aina 39 na kukatazwa zote. Baadhi ya kazi hizo ni:-
Kupika na kuoka (Kut. 16:23),
Kutembea siku ya sabato kuliruhusiwa kwa kiasi cha mwendo wa sabato tu, yaani
mita 938 au futi 3000 tu (Kut. 16:29),
Kuwasha moto (Kut. 35:3), Kukusanya
kuni (Hes. 15:32), Kulima na kuvuna
(Kut.34:21), Kuchukua mzigo iwe ni
kutoa au kuingiza ndani ya nyumba (Yer.17:21-23)
Kazi nyingine zilizokatazwa ni pamoja na kuwafunga watumwa, kupepeta,
kusafisha, kasaga, kukanda unga, kufua viatu, kusokota uzi, kufuma, kufanya
vifundo viwili, kuwasha moto, kugonga kwa nyundo na kubeba kitu kutoka eneo
moja hadi jingine. Aidha, siku ya sabato hakuna kupigana labda kwa kujitetea tu
baada ya kushambuliwa au kuvamiwa. Kuponya magonjwa yasiyonyeti na dharura kama
vile kupooza, ukoma au upofu zilikatazwa. Pale palipo na hatari ya kifo, msaada
ulihimizwa utolewe kwa haraka ili kifo kiepukwe. Hiyo ndiyo ilikuwa sabato na
kimsingi ndivyo ilivyo hadi leo hii kati ya waumini wa dini ya kiyahudi.
Kwa upande wa Yesu kama myahudi mwingine yeyote mwenye kuithamini dini
yake, aliiheshimu siku ya sabato. Alijumuika na wenzake kuhudhuria ibada
mbalimbali katika sunagogi. Hata hivyo Yesu hakuipokea tafsiri nzima juu ya
taratibu za mapumziko ya siku hiyo. Mafarisayo waligongana na Yesu mara nyingi
kwa sababu walimwona Yesu anakiuka sheria za kushika siku ya sabato.
Katika nafasi nyingi Yesu aliwaponya watu siku ya sabato. Sheria ilisema
mgonjwa asipate matibabu kamili siku ya sabato iwapo ugonjwa huo haukuhatarisha
maisha. Kwa mfano, mtu amepatwa na ajali ya kuvunjika mguu, sheria ilisema mtu
huyu ashughulikiwe kiasi cha kuufanya mguu wake usiharibike zaidi, lakini kazi
ya kuutengeneza kikamilifu na kuutibu lazima isubiri siku ya pili yake.
Matatizo ya ugonjwa aliyoyashughulikia Yesu kadiri ya wayahudi, hayakuwa ya
haraka wala muhimu kufanyika hata siku ya sabato. Ni sababu hiyo ilimfanya mkuu
wa sunagogi akasirike na kusema, “mnazo
siku sita za kufanya kazi. Basi fikeni siku hizo mkaponywe magonjwa yenu;
lakini msifike kwa ajili hiyo siku ya sabato.” (Rej. Lk. 13:14)
Jibu la Yesu kwa wapinzani wake ni kwamba, kumponya mtu siku ya sabato ni
tendo jema na hilo halina kizuizi cha wakati. Kila wakati ni wakati wa kutenda
mema. Kama wanyama wanasaidiwa siku ya sabato sembuse binadamu!
Muhtasari wa mafundisho ya Yesu kuhusu sabato ni huu, “Sabato iliwekwa kwa faida ya
binadamu na siyo binadamu kwa faida ya sabato” haya tunayasoma kutoka
Injili ya Marko 2:27.
Hiyo ndiyo sabato kati ya wayahudi na mtazamo wa Yesu juu ya sabato.
Sababu inayotufanya sisi wakatoliki na madhehebu mengine
ya kikristo tupumzike siku ya Jumapili na kuitakasa ambayo ni siku ya kwanza ya
juma badala ya Jumamosi ambayo ni siku ya saba ya juma.
Utamaduni wa kusali siku ya jumapili unapatikana tangu karne ya kwanza, yaani katika kipindi cha mitume wa
Yesu. Kanisa Katoliki na madhehebu yanayosali Jumapili yanafuata nyayo za
wafuasi wa kwanza wa Yesu Kristo. Yesu alipokufa mitume waliendelea na
utaratibu huo wa kushika sabato, wakati huohuo waliokutana siku ya kwanza ya
juma, yaani Jumapili, kwa lengo la kuumega Mkate, ikiwa ndiyo siku ile Yesu
alipofufuka. Polepole mambo yalianza kubadilika. Wayahudi walikuwa hawapendi
kuona kuwa wakristo nao wanashiriki nao katika Sinagogi au Hekaluni. Kwa sababu
walionekana kuwa na ajenda ya siri kwa kushiriki ibada mbili, yaani ile ya
Jumamosi (sabato}na ile ya Jumapili-siku ya kwanza ya juma. Wayahudi walitunga
ombi la kumi na mbili ambalo lilikuwa kwa ajili ya kuwalaani wakristo. Ombi
hilo lilikuwa ni kuwalaani wakristo ili majina yao yafutwe kwenye kitabu cha
uzima.
Uadui uliupoongezeka kati ya wayahudi washika sabato na wayahudi waliomwamini Kristo, waamini wa Yesu walifukuzwa
kutoka katika sinagogi, kama tusomavyo katika kitabu cha Matendo ya Mitume
18:16-18. Baada ya kufikia hatua hiyo, waamini wa Yesu walikutana mahali pao pa
sala napo palikuwa nyumbani kwa watu binafsi. Tunayapata haya katika kitabu cha
Matendo ya Mitume 18:7, pia 1Kor.16 na Rum. 16: 3-5. Humo waamini walisali,
walipata mafundisho kuhusu njia yao mpya na waliadhimisha Ekaristi Takatifu,
tendo lililoitwa wakati wa kumega Mkate. Hayo yote yalifanyika siku ya kwanza
ya juma, yaani Jumapili. (Rej. Mdo. 20:7). Kipindi ambacho haya yalifanyika ni
karne ya kwanza na wala siyo karne ya nne. Hivi, ieleweke kuwa kusali Jumapili
ni tendo lililoanza karne ya kwanza na wala siyo karne ya nne kama baadhi ya
watu wanavyotushutumu.
Hapa tunaweza kuanza
kuulizana kwa nini wafuasi wa Yesu walianza kufanya ibada siku ya Jumapili
badala ya sabato ambayo Bwana wetu Yesu Kristo aliiheshimu? Je, walifanya hivyo
kwa uhalali gani? Uhalali wa kufanya mabadiliko hayo, ulitokana na tukio kubwa
na la msingi kwa wanafunzi wa Yesu, yaani
ufufuko wa Yesu siku ya kwanza ya juma (Mt. 28:1; Lk. 24: 1; na Yoh. 20:1).
Umuhimu wa siku hiyo ni pamoja na ushindi wa
Bwana wetu Yesu Kristo dhidi ya maadui wawili yaani dhambi na mauti. Ilikuwa
pia siku ya kuleta matumaini makubwa kwa watu wote waliomwamini Yesu Kristo.
Uzito wa tukio hili unaelezwa vizuri sana na mtume Paulo “…kama Kristo
hakufufuka, basi, mahubiri yetu hayana maana na imani yetu haina
maana”(Rej.1Kor.15: 14). Kwa sababu ya umuhimu wa tukio la ufufuko wa Yesu,
siku ya ufufuko iliitwa siku ya Bwana (Ufu.1: 10). Katika lugha ya kilatini
siku ya Bwana huitwa Dominika.
Wafuasi wa Yesu waliona umuhimu wa kuienzi siku ya Bwana- yaani Dominika au
Jumapili wakaifanya kuwa siku ya kumega Mkate kama kumbukumbu ya siku ile ya
karamu ya mwisho.
Siku ya kwanza ya juma
ilikuwa pia ni siku ya kwanza ya enzi mpya ya maisha; kumsubiri Bwana wetu Yesu
Kristo kwa ujio wa pili wa kuwahukumu wazima na wafu.
Utamaduni huu wa kusali
Jumapili uliendelea miongoni mwa wakristo hadi karne ya nne, ulipopata nguvu
zaidi baada ya Kaisari Konstantino
kuitangaza Jumapili kuwa siku ya mapumziko katika dola yake. Kaisari
Konstantino katika vita na mpinzani wake Maxentius.
Usiku mmoja Kaisari Konstantino
aliota ndoto, akiwa katika ndoto aliona maono mfano wa msalaba halafu akasikia
maneno haya “katika ishara hiyo utashinda”. Hapo aliamua kubandika ishara ya
msalaba katika ngao za askari wake, hatimaye mwaka 312 aliweza kumshinda vitani
mpinzani wake katika daraja la Milvia
karibu na Roma. Tangu hapo ishara ya msalaba (ambayo ni ishara ya ushindi
dhidi ya mauti na kifo kutokana na kifo cha Kristo msalabani) ilipata heshima
ikawa ishara ya uzima. Kaisari Konstantino alizidi kuimarisha uhuru wa watoto
wa Mungu, pale alipotangaza Jumapili iwe
siku ya mapumziko kutokana na
ufufuko wa Yesu; siku iliyokuwa na uzito zaidi kuliko siku ile ya sabato,
yaani siku ya saba ya juma, ile ya Agano la kale. Konstantino alifanya haya
katika karne ya nne, wakati zoezi la kupumzika siku ya Jumapili lilikuwa
linafanywa na wafuasi wa Yesu tangu karne ya kwanza. Hivyo tusichanganye mambo
hapa kwa kusema kuwa kupumzika Jumapili kulianzishwa na Konstantino. Yeye
alichokifanya ni kutoa ruhusa rasmi katika dola yake katika tendo ambalo
wakristo walikuwa wakilifanya tangu karne ya kwanza.
Historia ya kupumzika
Jumapili si ndogo. Jinsi muda ulivyosonga mbele, miongoni mwa wakristo
wakatokea watu walioamua kurudi nyuma kwenda mpaka kwenye Agano la Kale, yaani
kupumzika na kuabudu katika siku ya kwanza ya juma, yaani Jumamosi.
Kwa maana hiyo utakuta
baadhi ya madhehebu ya kikristo yanaendelea kufuata maendeleo ya historia
yaliyohamishia sabato siku ya kwanza ya juma iliyo siku ya ufufuko wa Bwana,
ambayo ni sabato mpya na wapo wale walioamua kurudi nyuma kwenye sabato ya
kiyahudi yaani sabato ya Agano la Kale hawa ni wenzetu wasabato.
Maelezo ya jumla kufuatia maswali tunayoulizwa juu ya sabato
Sababu zinazotufanya sisi
wakatoliki tusali Jumapili ni hizi:
§ Sababu ya kwanza kubwa na ya msingi ni ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo
ambaye alifufuka siku ya kwanza ya juma, yaani Jumapili. Hili tunalipata katika
vifungu vifuatavyo: -Mt.28: 1; Lk. 24:1; Yn. 20:1. Hivi kufuatia umuhimu wa
tendo hili la kufufuka Yesu kristo, mitume na wakristo wa kwanza waliifanya
siku ya kwanza ya juma kuwa ndiyo siku ya mapumziko. Siku hiyo walipata
mafundisho kuhusu njia yao mpya na waliadhimisha Ekaristi Takatifu, tendo
lililoitwa kuumega Mkate, Rej. Mdo. 20:7. Tena kwa sababu ya umuhimu wa tukio
la ufufuko wa Yesu, siku hiyo ya kwanza ya juma iliitwa “siku ya Bwana” Rej.
Ufu. 1:10.
§ Pili, Yesu mwenyewe baada
ya ufufuko wake alikuwa akiwatokea wanafunzi wake katika siku ya kwanza ya
juma, yaani Jumapili,
§ Tatu, Roho Mtakatifu
aliwashukia mitume na watu waliokuwepo nao siku ya kwanza ya juma,
§ Nne, siku ya kwanza ya
juma ndiyo siku ambayo Mungu alianza kazi yake ya kuumba ulimwengu,
Maana ya msingi ya sabato ni kukoma, kuacha au
kupumzika kufanya kazi. Hivi sabato si Agano kama
wengine wasemavyo. Zaidi sana sabato si jina la siku fulani katika wiki. Sabato
ni kitendo cha kutenga siku fulani moja katika juma ili kumwabudu Mungu. Kwa
wenzetu wayahudi siku waliyokuwa wamemtengea Mungu, ilikuwa ni siku ya saba ya
juma na walikuwa na sababu zao za msingi.
Vigezo walivyotumia kuichagua siku ya saba ni:
(a)
Kukumbuka kitendo cha
kuondolewa kutoka utumwani Misri.
(b) Sabato ilikuwa ni alama kuwa Mungu aliliteua taifa la Isreli kuwa mali
yake.
(c)
Kuiga kile alichokifanya
Mungu, kwamba alipumzika siku ya saba, baada ya kumaliza kazi ya uumbaji.
Hivyo ndiyo vigezo
walivyotumia wayahudi katika uchaguzi wao wa siku ya saba ya juma.
Kanisa Katoliki
limeiga utamaduni huo wa kusali Jumapili au siku ya kwanza ya juma toka kwa
mitume waliofanya hivyo siku hiyo. Mmoja asifikiri kwamba ni viongozi wa Kanisa
ndio waliojitungia utaratibu au utamaduni huu katika kipindi fulani baada ya
mitume kufa, la hasha. Kanisa Katoliki linaushika utamaduni huu tangu nyakati
za mitume wa Yesu. Wengine wanadhani kulikuwa na mkutano fulani wa Kanisa Katoliki
uliojipitishia uamuzi wa kusali Jumapili, la hasha. Kwani Maandiko Matakatifu
yanaweka bayana kabisa jambo hili.
Watu wa kwanza
kupumzika siku ya Jumapili ni wafuasi wa kwanza wa Yesu, katika karne ya
kwanza. Kigezo kikubwa walichotumia ni ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo.
Ufufuko wa Kristo ndiyo kilele cha ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Ufufuko wa
Yesu ndio unaoleta maana hata katika kulisoma Agano la Kale. Yesu alipofufuka
ndipo watu walianza kusoma upya Agano la Kale na kupata maana sahihi ya ujumbe
wa Mungu kwa wanadamu. Hivi kwa yeyote anayetaka kusoma Biblia na kuielewa
vizuri, kiini cha yote ni ufufuko wa Yesu. Yesu mwenyewe anasema, “mwana wa mtu
anauwezo hata juu ya sabato”, (Rej. Mk. 2:28). Bila shaka wale wanaosali siku
ya kwanza ya juma wamechagua kilichobora zaidi, yaani Bwana Yesu, ambaye ni
Bwana wa sabato. Yeyote asiyeipokea siku ya ufufuko wa Yesu kwa namna ya juu
sana, huyo si mkristo. (Rej.1Kor.15:14). Siku ya ufufuko ndiyo inayotufanya
sisi sote leo tumfuate Kristo. Kama Kristo asingelifufuka bila shaka dini ya
kikristo isingekuwepo.
Katika Maandiko Matakatifu Mungu anasema ikumbuke siku ya
sabato na Kanisa linasema shika kitakatifu siku ya Bwana yaani Jumapili.
Ni kweli kabisa,
Kanisa Katoliki katika amri yake ya sita, linawaalika waamini wake kushiriki
Misa Takatifu siku ya Bwana na sikukuu zilizoamriwa. Ufufuko wa Yesu siku ya
kwanza ya juma-Jumapili ni uumbaji mpya. Mungu amependa kuumba upya ulimwengu
katika mwanae Yesu Kristo baada ya kuharibiwa na dhambi ya wazazi wetu wa kwanza
Adamu na Eva. Kama Mungu baba alivyoanza kuumba siku ya kwanza naye Yesu Kristo
ameumba ulimwengu upya siku ya kwanza ya juma ya ufufuko wake. Maana yake nini?
Maana yake ni kwamba siku ya kwanza ya juma, imekuwa siku yenye umuhimu zaidi
kuliko sherehe na sikukuu zote zinazofahamika hapa duniani.
Zaidi ya hayo,
Jumapili (siku ya kwanza ya juma) ndiyo inayoikamilisha maana nzima ya siku ya
sabato na kututangazia sisi wanadamu pumziko la milele katika Mungu. Kristo
mwenyewe alisema, “msidhani kuwa nimekuja kutengua sheria na mafundisho ya
manabii. Sikuja kutengua bali kukamilisha”(Mt. 5: 17). Vile vile sabato ni
kivuli tu, ukweli wenyewe ni ufufuko wa Yesu siku ya kwanza ya Juma- yaani
Jumapili.
Mtume Paulo anaeleza
vizuri sana juu ya ukweli huu, “Kwa hiyo basi msikubali kupewa masharti na mtu
yeyote kuhusu vyakula au vinywaji, siku ya sherehe, sikukuu ya mwezi mpya au
sabato. Mambo ya aina hiyo ni kivuli tu ya yale yatakayokuja, ukweli wenyewe
ndiye Kristo”
Kufuatia maelezo haya,
unaweza kuona kuwa kamwe Kanisa Katoliki halipingani na Mungu, bali lipo upande
wa Mungu na kutangaza ukweli huu kwamba, Kristo alifufuka na ufufuko wa Kristo
ni ukamilifu wa Mungu katika kumkomboa binadamu dhidi ya dhambi na mauti.
Kumpinga Mungu ni kwenda kinyume na mapenzi ya Mungu.
THE END
Nb: Sehemu ya majibu haya ni kutoka kwenye Maandiko Matakatifu, pia Seminari Kuu Peramiho katika vipindi cha Radio Maria Songea.
UKIWA NA MASWALI USISITE KUTUMA KATIKA BLOG HII (Kwa lugha ya English na Kiswahili).
No comments:
Post a Comment